Kampuni za madini zaonywa kuajiri watoto migodini

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 06:02 AM Apr 19 2024
Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Judica Omari.
Picha: Maktaba
Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Judica Omari.

SERIKALI mkoani Njombe imetoa onyo kwa kampuni za uchimbaji madini mkoani hapa kuepuka tabia ya kuwaajiri watoto.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Judica Omari wakati akifungua mafunzo kwa wadau na wachimbaji wa madini yaliyoandaliwa na Tume ya Madini mkoani hapa.

“Tuangalie ajira tunazotoa ziwe nzuri zenye manufaa na zenye faida kwa wote, tusiende tukatumie ajira kwa watoto haitakiwi. Kuna baadhi ya stori kwenye migodi baadhi inatumia watoto wadogo,” alisema Omari.

Aidha, alitoa rai kwa wanawake mkoani hapa kuchangamkia fursa mbalimbali ambazo zinapatikana kwenye migodi sambamba na kuingia ubia na kampuni ambazo zinavifaa vya kuchimbia.

Alisema sekta ya madini katika pato la taifa linachangia asilimia tisa kutoka asilimia nne kwa kipindi cha miaka ya nyuma.

Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Njombe, Zabibu Napacho alisema katika Mkoa wa Njombe yapo madini ya kimkakati kama dhahabu, makaa ya mawe na shaba.

“Pamoja na shughuli za madini lakini Mkoa wa Njombe una leseni 400 lakini leseni ambazo zinafanya kazi ni 40 tu kwa hiyo tunahitaji kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha ili kila mmiliki ajue wajibu wake,” alisema Napacho.

Alisema kuwa katika mkoa huo pia kuna ongezeko la makusanyo kuanzia mwaka wa fedha 2017 ambao tume imeanza kazi hadi mwaka 2024.

Alisema kwa mwaka wa fedha ulioanza Julai lengo la makusanyo lilikuwa Sh. bilioni 3.85 ambapo hadi sasa wamekusanya Sh. bilioni 3.5 sawa na asilimia 91.