Mavunde ateta na uongozi wa Mamba Minerals, awataka kufuata masharti ya leseni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:47 PM Apr 18 2024
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (kulia) akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Kampuni  ya Peak Resources Ngualla Company ya nchini Australia ( PRNG) Bardin Davis (kushoto).
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (kulia) akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Peak Resources Ngualla Company ya nchini Australia ( PRNG) Bardin Davis (kushoto).

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amekutana na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Peak Resources Ngualla Company ya nchini Australia ( PRNG) Bardin Davis, yenye umiliki wa hisa asilimia 84 kwenye mradi wa Uchimbaji Madini Mkakati ya Rare Earth Elements.

Katika kikao hicho kilichofanyika  leo Aprili 18, 2024 jijini Dodoma, Bardin ameambatana  na Afisa Mkuu   wa masuala ya Fedha ya kampuni hiyo, Phil Rundell,  pamoja na Mkurugenzi wa Mamba Minerals Corporation  Limited ( MML)   yenye ubia na Serikali, Ismail Diwani.

Katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa PRNG Bardin amemweleza Waziri Mavunde kuhusu maendeleo ya mradi huo na kueleza kuwa  hivi sasa upo katika hatua ya kufanya tathmini ya fidia ya wananchi wanazunguka mgodi ikiwemo uendelezaji wa utafiti wa madini ya mkakati aina ya niobium, fluorspar na phosphate. 

Aidha, Bardin ametumia kikao hicho  kuishukuru wizara kupitia Tume ya Madini kwa  kuridhia kuongeza ukubwa wa leseni ya kampuni hiyo.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mavunde ameusisitiza uongozi wa kampuni  hiyo  kufuata masharti ya leseni  waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuzingatia matakwa ya Sheria ya Madini na kusisitiza kuhusu umuhimu wa madini hayo  kusafishwa hapa hapa  nchini.

Madini ya rare earth elements  yanayotumika kutengeza sumaku kwenye mota za magari ya umeme , betri za magari ya mseto na umeme;na  vitu vingine  mbalimbali vya umeme. 

Kampuni ya Mamba Minerals  inayomiliki leseni kubwa ya uchimbaji  yenye jina la Rare Earth Elements ilitolewa tarehe 25 Aprili, 2023.

Mradi wa uchimbaji madini hayo upo kijiji cha Ngualla, Mkoani Songwe.

Katika mradi huo, Serikali ya Tanzania ina miliki  asilimia 16 za hisa zisizohamishika.