Kesi ya msanii Marioo madai ya milioni 500/- kuunguruma

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 11:30 AM Mar 18 2024
Marioo.
PICHA: MTANDAO
Marioo.

MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Omary Mwanga, maarufu Marioo, anayedaiwa zaidi ya Sh. milioni 500 kwa kuvunja mkataba, anatarajiwa kujitetea Mahakama Kuu Machi 18 na 19, mwaka huu.

Marioo na Meneja wake Sweetbert Mwinula wameshtakiwa katika Mahakama Kuu Masjala ya Wilaya ya Arusha mbele ya Jaji Joackim Tiganga, wakidaiwa jumla ya Sh. 550,000,000 kwa madai ya kuvunja mkataba wa kutumbuiza katika hafla ya Mr & Miss Vyuo Vikuu Kanda ya Kaskazini.

Mdai katika shauri hilo ni Kampuni ya Kismaty inayojihusisha na kuandaa matukio ya burudani mbalimbali nchini.

Mdai anayewakilishwa na Wakili John Lairumbe, anadai kuwa Septemba 23, 2021, aliingia mkataba na wadaiwa kutumbuiza siku ya mashindano hayo kwa gharama ya Sh. milioni 15.

Mdai anadai katika hati yake ya madai kwamba tukio lilitakiwa kufanyika Septemba 24, 2021 Arusha na Septemba 25 mwaka huo kungekuwa na hafla iliyopangwa kufanyika Blue Stone Lounge.

Anadai kuwa kampuni hiyo Septemba 17, mwaka huo, iliwalipa wadaiwa Sh. milioni nane na wakati wakitia saini mkataba, iliwalipa Sh milioni 15.

Inadaiwa kuwa Septemba 25, 2021, hawakuonekana kwa ajili ya kutumbuiza Blue Stone kama walivyokubaliana katika mkataba.

Kutokana na kuvunja mkataba, mdai aliingia hasara ya Sh. 500,000,000 na hasara nyingine ya Sh. 50,000,000 ambayo ilitokana na kukaribisha wadau mbalimbali wakiwamo wenye hoteli kubwa, fedha walizolipwa na alipoteza biashara na kukosa kipato.