Watu 40 wafariki dunia baada ya bwawa kupasua kingo zake Kenya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:00 PM Apr 29 2024
Athari baada ya bwawa kupasua kingo zake nchini Kenya.
PICHA: BBC
Athari baada ya bwawa kupasua kingo zake nchini Kenya.

ZAIDI ya watu 40 wamefariki dunia baada ya bwawa kuvunja kingo zake katika eneo la Mai Mahiu Kaskazini mwa Mji Mkuu Nairobi nchini Kenya, Shirika la Msalaba Mwekundu nchini humo limeithibitisha.

Gavana wa eneo hilo, Susan Kihika naye alithibitisha vifo hivyo kwa shirika la habari la AFP, na kuongeza kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka.

Mashuhuda wamesimulia kuwa, maji yalitiririka na kusomba nyumba na magari kadhaa katika kijiji cha Kamuchiri, kufuatia mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha katika maeneo kadhaa nchini humo.

BBC meripoti kuwa, vikosi vya uokoaji vinachimba matope kutafuta manusura, vyombo vya habari vya eneo hilo vimesema, huku vikionya kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa.

Mvua hiyo imepasua barabara kuu kutoka Nairobi kuelekea Mai Mahiu baada ya mawe makubwa, matope na magogo kuziba eneo hilo.

Mapema leo Jumatatu, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limesema kuwa tayari wamewapeleka watu kadhaa katika kituo cha afya huko Mai Mahiu kutokana na mafuriko.

Vifo vya hivi punde vinafanya idadi ya watu kutokana na mvua kubwa na mafuriko nchini tangu mwezi uliopita kuongezeka.

BBC