6 mbaroni tuhuma kujihusisha mikopo kausha damu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:30 PM May 06 2024
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Songwe, Augustino Senga.
PICHA: MAKTABA
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Songwe, Augustino Senga.

JESHI la Polisi mkoani Songwe kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), limewakamata watuhumiwa sita wanaojihusisha na utoaji wa mikopo ya kausha damu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Songwe, Augustino Senga, amesema watu hao wamekamatwa wakifanya biashara ya kutoa mikopo bila ya kuwa na leseni kinyume cha Sheria ya Mikopo Midogo Namba 10 ya Mwaka 2018, Kifungu cha 16.

Senga amesema watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya Jeshi la Polisi kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu huduma za mikopo midogo maarufu kama kausha damu wanayoifanya.

Amesema baada ya kupokea malalamiko hayo waliendesha operesheni ya kukusanya ushahidi na kuwakamata wamiliki wa kampuni na watu binafsi wanaotoa huduma za kifedha pasipo kuwa na leseni.

Kamanda Senga amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria na atakayepatikana na hatia atalipa faini isiyopungua Sh. milioni 20, lakini isiyozidi Sh. milioni 100 au kifungo kisichopungua miaka mitano jela.

Kadhalika, amewakumbusha watoa huduma wa mikopo midogo kufuata taratibu za usajili na miongozo iliyowekwa na BoT ili kuepuka usumbufu unaotokana na kutotii sheria.

Vilevile, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuwabaini na kuwakamata wafanyabiashara ambao wanaochukua kadi za benki kama dhamana ya mikopo hiyo kinyume cha sheria.

Katika tukio lingine, Kamanda Senga amesema Jeshi la Polisi liliwakamata watuhumiwa sita kwa tuhuma za kughushi barua ya kusitishiwa mikataba ya kazi ikiwa na mihuri ya taasisi binafsi na za serikali pamoja na fomu za kuchukulia mafao ili waweze kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa Februari 22, mwaka huu na upelelezi wa mashauri haya bado unaendelea na utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.

SERIKALI YAHADHARISHA

Hivi karibuni serikali kupitia Ofisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Salim Kimaro, imetoa wito kwa watoa huduma za kifedha nchini kufuata sheria na taratibu za huduma za fedha ikiwamo kupata leseni ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa ufanisi bila kuwaumiza na kuwadhalilisha wanufaika na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.

Benki hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha imeona umuhimu wa kutoa elimu ya fedha nchi nzima ili kuwapa uelewa wananchi kuhusu namna bora ya kukopa fedha na kurejesha mkopo bila kudhalilishwa.

Serikali imebaini kuwa mikopo inayotolewa kwa njia ya mitandao ya simu ni changamoto kubwa hasa katika ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wakopaji jambo linalosababisha watoa huduma hao kuvunja sheria ya usiri inayotakiwa katika kupata huduma ya fedha kwa kuwadhalilisha wakopaji hao kwa kutuma ujumbe mfupi kwa ndugu na jamaa waliochukua mikopo hiyo. 

‘’Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania tunahitaji kushirikisha, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, kampuni za simu na Polisi ili kuona namna ambayo tunaweza kulitatua suala hili la udhalilishaji linalofanywa na watoa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu,’’ imesema serikali kupitia ofisa huyo.

Aidha, Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania hivi karibuni itaendesha kampeni kupitia vyombo vya habari na njia mbalimbali za kutoa elimu kwa umma ili kujenga uelewa kwa wananchi na watoa huduma ndogo za fedha kuhusu masuala muhimu ya kuzingatia katika utoaji na upatikanaji wa huduma ndogo za fedha nchini.

WAATHIRIKA MIKOPO UMIZA

Waathirika wa mikopo hiyo watajwa kuwa ni wastaafu na walimu kutokana na madai ya kipato wanachopata kutoridhisha na hivyo kujiingiza kwenye mikopo hiyo na mwishoe kuishia udhalilishaji.

Hivi karibuni mjadala uliibuka bungeni kutoka kwa wabunge wakilaani mikopo hiyo na kuta serikali ichukue hatua za haraka.

Kadhalika, amesema Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa 11 kwa makosa ya wizi wa pikipiki nne, pamoja na kuwakamata watuhumiwa wengine 14 kwa makosa ya uvunjaji.

Pia, amesema Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa 424 kwa kujihusisha na matukio ya ukatili wa kijinsia, uvunjaji, wizi, mauaji, utapeli kwa njia ya mtandao, kujifanya mtumishi wa serikali, kughushi nyaraka, dawa za kulevya, ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.