Hoja 16 THTU uboreshaji wa kikikotoo, NHIF

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:03 PM Apr 25 2024
Mwenyekiti wa THTU Taifa, Dk. Paul Loisulie.
PICHA: MAKTABA
Mwenyekiti wa THTU Taifa, Dk. Paul Loisulie.

IKIWA zimesalia siku kadhaa kufikia maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi), Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU), kimefanya uchambuzi na kutoa mapendekezo 16 kuhusu hoja za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na kikokotoo cha mafao ambacho kimekuwa kikilalamikiwa na watumishi wa umma nchini.

Mwenyekiti wa THTU Taifa, Dk. Paul Loisulie, akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, amesema vikwazo vilivyopo kwenye mfuko huo na pensheni vinaathiri haki za mfanyakazi kupata stahiki husika pindi anapostaafu.

Kuhusu kikokotoo, Dk. Loisulie amesema kanuni inayotumika haiakisi hali halisi ya wanachama kwa kanuni 8(1) (a) (b) (c) inayozungumzia kigezo cha umri na malipo ya mkupuo. Alisema wakati umri wa kuishi wa Mtanzania umeongezeka, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na makazi ya Mwaka 2022, mafao kwa mkupuo kwa mwanachama yanakuwa ni madogo.

“Madhara yake ni kwamba kupunguza umri wa kuishi baada ya kustaafu kunapunguza pensheni ya mwanachama na kupungua kwa morali  ya wanachama na watu kukimbia utumishi wa umma,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, amependekeza kikokotoo kifanyiwe mabadiliko kwa kuongeza umri baada ya kustaafu kutoka miaka 12.5 hadi 15.5 na wanachama wapewe angalau asilimia 50 kama mafao ya mkupuo. Pia alishauri  itumike kanuni ya 1/540 badala ya 1/580.

Pia amesema THTU imebaini waziri husika ana mamlaka ya kuamua kiwango cha michango ya mwanachama katika mfuko kupitia kifungu Na. 18, hivyo mamlaka aliyopewa waziri yakitumiwa vibaya yatakuwa kandamizi kwa wanachama.

Amependekeza kifungu kidogo cha 18(2)(b) kiondolewe na kionyeshe kuwa waziri hapaswi kuwa na mamlaka ya kupanga michango ya wanachama.

Kadhalika, amesema kifungu na 39 kinachohusu wajane, wagane na watoto wana haki ya kunufaika na mafao ya mwanachama aliyekuwa wakimtegemea kwa muda wa miaka mitatu pekee kutoka tarehe ya kifo cha mwanachama, kinasababisha familia kukosa huduma stahiki na kupendekeza walipwe angalau kwa miaka 15.

“Kifungu cha 18 (a) kinamyima mnufaika haki yake ya kikatiba ya kuoa au kuolewa, Neno until “re-marriage” linapaswa liondolewe ili kulinda haki ya kikatiba ya kuoa na kuolewa pasipo na vikwazo. Mjane,mgane aruhusiwe kupata mafao bila ya vikwazo vya umri na kuwa na mtoto,” amesema.

Pia amesema kifungu na 40 kuhusu wanachama katika mfuko mmoja kuwa na kanuni tofauti za kukokotoa mafao ni kutengeneza matabaka katika jamii na kupendekeza kuwepo na masharti yanayofanana kwa wanachama wote ili kuondoa ubaguzi na kigezo cha mshahara  mkubwa kitumike kwenye mafao.

Kuhusu mwanachama kupunjwa mafao kwa kosa la mwajiri, amesema kifungu cha 20 kinazungumzia Mwajiri anaposhindwa kuwasilisha michango ya mwanachama kwa wakati au kutowakilisha kabisa. Kifungu hakimlindi mwanachama iwapo mwajiri amechelewesha au hakupeleka michango kwenye mfuko na kusababisha kupunjwa mafao.

“Tunapendekeza kiongezwe kifungu kidogo maalum kitakacholinda haki za mwanachama moja kwa moja iwapo mwajiri atachelewesha au kutopeleka mchango wa mwanachama katika mfuko na  mwanachama alipwe mafao yake yote na mfuko umdai mwajiri michango iliyokosekana pamoja na penati,”amesema.

MAPENDEKEZO NHIF

Amesema kifungu 16(3) cha Sheria ya Bima ya Afya kinamtaka mnufaika kuchangia gharama za ziada za matibabu lengo likiwa ni kuuondolea mfuko wajibu wake wa kisheria wa kulipia gharama za matibabu. Alisema hali hiyo inampa mwanachama mzigo na inaathiri huduma ya matibabu kwa mnufaika, hivyo kumfanya kutokuona umuhimu wa kuwa na bima ya afya.

“Kifungu cha 16(3) cha Sheria ya Bima ya Afya kiboreshwe kwa kuupa mfuko wajibu wa kumlipia mwanachama huduma zote stahiki kutokana na mahitaji ya ugonjwa wake kwa ubora unaostahiki,” amesema.

Kuhusu mabadiliko ya wigo wa upatikanaji wa huduma ya bima mara kwa mara, amependekeza Kifungu cha 16(4) cha Sheria ya Bima ya Afya kirekebishwe kwa kutaka mabadiliko ya vitita vya matibabu yafanyike kwa kuwashirikisha wadau ambao ni watoa huduma na wanufaika au wachangiaji.

Amependekeza miongozo ya upangaji wa gharama za matibabu iwe shirikishi na izingatie uhalisia wa utoaji wa huduma husika na mchangiaji apewe uhuru wa kuamua wategemezi anaotaka wanufaike na bima bila kuathiri ukomo wa idadi kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 3 cha sheria ya Bima ya Afya.

Amesema kunahitajika majadiliano kutokana na kutokuwa na usawa katika kupata huduma kwa wanufaika wa huduma ya bima, yaani wabunge na watumishi wa umma.

“Tunapendekeza mfuko ufuate matakwa ya kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Bima ya Afya ambacho kimetaja makundi ya watu wanaoweza kujiunga na Bima ya Afya ambaio ni watumishi wa umma, wenza wao, Watoto au wategemezi, wastaafu na madiwani. 

“Hata hivyo, kinyume cha sheria inavyotaka, kwa sasa sheria imeongeza wigo wa wanachama wa Bima ya afya kama vile wabunge, mashirika binafsi, watoto, wanafunzi wa vyuo,” amesema.

Amependekeza Mfuko uwashirikishe wadau kikamilifu wakati wa upangaji wa gharama za huduma na kuwe na chombo mahsusi cha kudhibiti gharama za huduma za bima za afya.

“Tunashauri tathmini ifanyike ili kuona kama viwango vya michango inayotolewa sasa ina uhalisia na gharama za matibabu wanazopata wanufaika. Tunashauri serikali iweke tengo maalum kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato kutoka kwenye rasilimali tulizonazo ili kuutunisha na kuuimarisha Mfuko,” amesema.

Katika  kuhakikisha kunakuwapo na uhai wa mfuko huo, alipendekeza fedha za mfuko zitumike kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.