Mafundi ujenzi, mkulima mbaroni madai ya mauaji

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 08:56 AM May 04 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama.

JESHI la Polisi mkoani hapa linawashikilia watu watatu wakiwamo mafundi ujenzi kwa tuhuma za mauaji ya mfanyakazi wa ndani, Monica Paul (22), mkazi wa Mtaa wa Lukuyu, Kata ya Bigwa, katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Mtuhumiwa mwingine, Rehema Omary (30), mkulima na mkazi wa Mwembesongo, anadaiwa kukutwa na  simu ndogo ya marehemu aina ya TECNO.

Inadaiwa watuhumiwa hao walitekeleza mauaji hayo katika nyumba iliyoko Lukuyu-Bigwa baada ya kufika na kuanza kuiba vitu, mfanyakazi huyo katika kutetea ndipo walipomuua.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, alisema tukio hilo lilitokea Aprili 14, mwaka huu, usiku ambapo watuhumiwa wawili ambao ni mafundi ujenzi walikuwa wakitumiwa na mmiliki wa nyumba hiyo aishie Dar es Salaam, kufanya matengenezo nyumbani hapo.

Aliwataja mafundi hao ni Mbaraka Omary (25), mkazi wa Tubuyu, ambaye amekutwa na vielelezo TV aina ya Hisence inchi 60,  redio sabufa aina ya Boss, spika ndogo za redio hiyo na feni nyeupe ndogo aina ya Easy Home ambavyo vyote viliibiwa siku ya tukio.

Kamanda alimtaja fundi mwingine kuwa  ni Mussa Mrisho (23), mkazi wa Bigwa, ambaye anadaiwa alishirikiana na mwenzake kutekeleza mauaji hayo, wakati mtuhumiwa Rehema Omary (30), mkulima, mkazi wa Mwembesongo, alikutwa na simu ndogo ya marehemu aina ya Tecno.

“Hawa mafundi walitumia mwanya huo wakitambua binti huyo ni dhaifu alikuwa peke yake na baada ya kufanya mazoea, Aprili 14, mwaka huu, walikwenda hapo nyumbani usiku kufanya tukio la mauaji yake,” alisema.

Alisema watuhumiwa walifika usiku na kumgongea mlango mfanyakazi huyo naye alifungua kwa kuwa ni watu ambao anawafahamu, alipofungua wakaanza kuiba mali zilizokuwamo ndani, na wakati wa kunyang’anyana ndipo tukio la kumuua likafanyika.Kutokana na tukio hilo, Kamanda Mkama alitoa tahadhari kwa wananchi kutumia mafundi ujenzi wanaofahamika ili kuepusha vitendo vya kihalifu, huku akiwaomba wananchi kutoa taarifa za wahalifu ili zifanyiwe.