Kampeni mlango kwa mlango TRA yavuna mabilioni

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 09:31 AM May 02 2024
Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Hudson Kamoga.
PICHA: MAKTABA
Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Hudson Kamoga.

KAMPENI ya mlango kwa mlango inayoendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), imechangia kwa kiasi kikubwa kupaisha mapato yanayokusanywa na mamlaka hiyo.

Kwa mujibu wa TRA, Desemba, mwaka jana, iliweka historia kwa kukusanya Sh. trilioni 3.05 kwa mwezi wakati lengo lilikuwa  kukusanya Sh. trilioni 2.9 kwa mwezi, sawa na ongezeko la asilimia 9.2.

Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Hudson Kamoga,  amesema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa 13 wa kitaaluma wa wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) unaoendelea jijini hapa. 

Amesema kampeni ya mlango kwa mlango imechangia kwa kiwango kikubwa wananchi kuelewa umuhimu wa kulipa na imesababisha ongezeko la walipakodi kwa hiari na kwamba wameachana na matumizi ya nguvu.

“Moja ya sababu za kuongezeka kwa makusanyo ni mwamko mkubwa wa ulipaji kodi kwa wafanyabiashara na tumekuwa tukitumia mbinu bora na rafiki za ukusanyaji wa mapato na tulishaachana kabisa na matumizi ya nguvu kudai kodi,”  amesema.

Kamoga  amesema ongezeko la uwekezaji na ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini ikiwamo uzalishaji viwandani, uingizaji wa bidhaa na kuimarika kwa shughuli za utalii ni miongoni mwa vichocheo vya ukuaji wa ukusanyaji wa mapato kwa mamlaka hiyo.

Amesema filamu ya The Royal Tour ambayo Rais Samia Suluhu Hassan alishiriki kuitengeneza, imechangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka makusanyo ya mapato kwenye sekta ya utalii hasa kwenye kodi ya ongezeko la thamani (VAT), ada za utalii na kodi ya mapato kwa kampuni zinazojihusisha na utalii.

Mkurugenzi huyo  amesema uboreshaji wa uhusiano baina ya mamlaka na walipakodi, utatuzi wa migogoro ya kodi nje ya mahakama na kuongezeka kwa kiwango cha uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa njia mbalimbali nako kumechangia ongezeko la mapato.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu (2021-2023), kiwango cha wananchi na walipakodi kutii na kufuata sheria, kimeongezeka kwa upande wa matumizi ya huduma ya kuhakiki stempu ambapo kiwango cha kupakua kimeongezeka na kufikia 508,3000 kwa watumiaji wa simu za ‘androids’ na ‘IOS’.

Kuhusu mashine za kielektroniki (EFD), Kamoga alisema  mfanyabiashara yeyote anayejihusisha na kuuza bidhaa au huduma, anatakiwa kwa mujibu wa sheria kununua mashine hiyo au VFD kutoka kwa mawakala walioidhinishwa na mamlaka hiyo.

Amesema baada ya kununua mashine hiyo, mfanyabiashara anatakiwa kuitumia mashine hiyo kutoa risiti kila anapofanya biashara ili kuhakikisha anawatendea haki wateja wake kwa kuwapa risiti sahihi.

Kamoga amesema awamu ya kwanza ya matumizi ya mashine hizo, ilianza Julai, 2010 na ilihusisha wafanyabiashara waliosajiliwa na  VAT na kwamba mwaka 2013 na awamu ya pili ilianza ikihusisha wafanyabiashara wasiosajiliwa kwenye VAT ambao mauzo yao ghafi ni shilingi milioni 14 kwa mwaka.

Amesema kuanzia Februari, 2022 kiwango cha mauzo ghafi cha mfanyabiashara kwa ajili ya kununua mashine za kielektroniki kilishushwa kutoka Sh. milioni 14 hadi milioni 11 kwa mwaka.