Leseni, matumizi kikoa cha taifa vyaongezeka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:35 PM Apr 25 2024
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabiri Bakari.
PICHA: MAKTABA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabiri Bakari.

LESENI za huduma za utangazaji Tanzania zimeongezeka kati ya asilimia tano na 350 kwa aina tofauti kati ya Desemba 2023 na Machi 2024, huku taasisi zaidi zinatumia kikoa cha Tanzania kwenye mawasiliano yao mtandaoni, taarifa ya hivi karibuni imeonesha.

Taarifa ya hali ya sekta ya mawasiliano iliyotolewa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabiri Bakari, inaonyesha kuwa leseni za usafirishaji vifurushi kati ya miji kwenye mikoa zimeongezeka kwa asilimia 30 ni za mabasi ya abiria. 

Ripoti hiyo imeeleza kuwa leseni za kitaifa za huduma za maudhui ya televisheni za kulipiwa (shitariki) ziliongezeka kwa asilimia 60 kutoka 10 hadi 16 na leseni za wilaya kwa kundi hili zimeongezeka kwa asilimia 350 kutoka mbili hadi tisa kati ya Desemba, 2023 na Machi, mwaka huu.

“TCRA ilitoa leseni 17 za redio za jamii kati ya Januari na Machi 2024, kulinganisha na 11 kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2024 ambazo ni ongezeko la asilimia 55. Leseni hii inawezesha utoaji huduma za utangzaji mwa jamii au watu waliojumuika sehemu moja kijiografia,” amesema.

Kwa mujibu wa kanuni za maudhui ya redio na televisheni, watangazaji wa kundi la leseni za jamii wanatoa kwa jamii husika maudhui yanayohusu masuala ya jamii hiyo ambayo kwa uzoefu hayatolewi na watoa huduma wengine wa maudhui wanaofikisha huduma maeneo vilipo vituo vya jamii.

Aidha, taarifa hiyo imeonyesha kuwa vikoa vya taifa vinavyoishia na dot ‘tz’ vilivyosajiliwa vimeongezeka kutoka 29,006 mwishoni mwa Desemba 2023 hadi 29,968 mwishoni mwa Machi, 2024. 

“Taasisi na watu binafsi wanazidi kutumia kikoa cha Tanzania kwenye vovuti zao na barua pepe.Kikoa ni jina mahsusi linalotambua raslimali za intaneti kama vile tovuti zilizosajiliwa kwenye nchi husika na ngazi nyingine duniani,”amesema.

Pia imebainisha kuwa vikoa vya kampuni na biashara (dot ‘co’), taasisi za elimu zenye ithibati (dot ‘ac’) na mashirika yasiyotegemea faida kwenye shughuli zao (dot ‘or’) zimeongezeka zaidi kipindi hicho.

“TCRA inahimiza matumizi ya kikoa cha taifa kinachoishia na kifupisho cha Tanzania, yaani dot ‘tz” kwenye maelezo na shughuli za taasisi. Vikoa vya taifa vina faida zaidi ya vile vya jumla kwa kuwa vinatambulisha taasisi na nchi husika. Vilevile vinajenga imani ya watumiaji wa tovuti ya mwenye kikoa,”imesema taarifa hiyo.