LHRC yashauri sheria itungwe kuwalinda wanawake na watoto

By Enock Charles , Nipashe
Published at 01:25 PM Apr 25 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga.
PICHA: MAKTABA
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga.

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimependekeza kutungwa sheria kulinda makundi maalum wakiwamo wanawake na watoto dhidi ya ukatili.

Mapendekezo hayo yanatokana na taarifa ya kituo hicho kwa mwaka 2023 kuonyesha kuwa makundi hayo ndiyo yaliyoathirika zaidi dhidi ya vitendo hivyo.

Akizungumza katika uzinduzi wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2023, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga,  amebainisha kuwa robo tatu ya manusura wa ukiukwaji wa haki za binadamu walikuwa watoto asilimia 45 na wanawake asilimia 30, huku manusura wengine wakiwa ni wazee (asilimia 12) na watu wenye ulemavu.

“Watoto na wanawake ni waathirika wakubwa wa ukiukwaji wa haki za binadamu na baadhi ya mikoa ambayo imeongoza kwa ukiukwaji wa haki hizo ni Dar es Salaam, Njombe, Geita, Arusha, Kilimanjaro, Mara, Kigoma na Dodoma” amesema Dk. Henga.

Kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo, Dk. Henga amelitaka jamii kutokufumbia macho pale inapoona ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu vinafanyika hasa kwa Watoto.

Amesema mara nyingi vitendo hivyo hufanywa na watu wa karibu na mtoto kama vile mjomba, baba, baba mdogo, babu hata mama mzazi, hivyo kuwa vigumu kuripotiwa katika vyombo vya ulinzi na usalama.

Ripoti hiyo pia imefichua kuongezeka suala la mauaji ya kujichukulia sheria mkononi kwa wananchi wanaokamatwa kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya wizi pia mauaji ya wenza kwa kile kinachodaiwa wivu wa kimapenzi na imani za kishirikina.

“Masuala mengine yaliyoainishwa katika ripoti hii ni mauaji yanayotokana na wananchi kujichukulia sheria mkononi, mauaji yanayotokana na imani za kishirikina na mauaji ya wenza baina ya wenza hao kwa mmoja kumuua mwenzie kwa wivu wa mapenzi,” amesema Dk. Henga

Mbali na haki za watoto na wanawake, ripoti hiyo ilibainisha pia ukiukwaji wa haki katika kundi la waandishi wa habari ukiwamo wa kiuchumi kwa kutokupewa mikataba ya kazi na fedha zao kutokupelekwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii huku wengine wakilipwa ujira mdogo wa kazi zao, hivyo kutaka  waajiri kujirekebisha.