Makahaba Shinyanga walia njaa

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 03:05 PM Apr 25 2024
Makahaba Shinyanga walia na njaa.
PICHA: MAKTABA
Makahaba Shinyanga walia na njaa.

BAADHI ya wakazi wa Kata ya Mwamala Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa, wameiomba serikali kuzinusuru familia zao kufa kwa njaa kutokana na waume zao kuhonga makahaba magunia ya mpunga katika kipindi cha mavuno na kusababisha wao na watoto kukosa chakula.

Mkazi wa Kijiji cha Mwamala 'B', Salima Sosoma alitoa ombi hilo wakati akizungumza na NIPASHE katika utekelezaji wa mradi wa wanajamii na vyombo vya habari katika kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto unaofadhiliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT).

Salima, amesema katika maeneo ya vijijini  kuna idadi kubwa ya wanawake kutoka mjini wanaojifanya wanauza vileo huku wakiwa wanauza miili yao kwa ujira wa kubadilisha kuanzia debe moja la mpunga hadi gunia kwa vijana na waume zao hali inayosababisha familia zao kukosa chakula.

“Kama unavyojua sie wanawake wa Kisukuma hatuna sauti mbele za wanaume zetu na ukijifanya mjuaji unaadhibiwa mbele ya watoto, tunaiomba serikali iingilie kati na kuwaondoa madada poa ambao wengi wao wanafukuzwa mjini na kukimbilia vijijini kutapeli mazao yao,” amedai..

Ester Kenedy, amesema wanaendelea na uvunaji wa mazao mchanganyiko, ikiwemo mpunga na inapofika nyakati za usiku eneo la katikati ya kata hiyo ambako kuna mzunguko mkubwa wa biashara utakuta madada hao wamejaa kwenye kumbi za starehe ikiwemo zinazouza vileo.

Amesema wanaiomba serikali kuingilia kati na kuwanusuru na janga la njaa ambalo linaweza kutokea baada ya waume zao kujiingiza kwenye ukahaba kwa kuwalipa mazao hayo badala ya fedha.

Amesema wamekuwa wakiona kwenye vyombo mbalimbali vya habari namna serikali inavyowaondoa mitaani makahaba hao na kuwanusuru vijana na kuvunjika kwa ndoa.

“ Mbinu inayotumia kuwoandoa makahaba mjini basi itumike pia kuwaondoa vijijini na itasaidia  kupunguza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi katika ndoa na baadhi ya vijana,” amedai.

Ofisa Kilimo wa Kata hiyo, West Mwanda amethibitisha baada ya chakula kuisha kwenye familia wanaoteseka ni  wanawake na watoto.

Mwanda, amesema amekuwa akikemea tabia hiyo mara kwa mara hasa anapowatembelea wakulima  kuwaelimisha kilimo cha kisasa cha mazao ya chakula na biashara.

Amesema hali ya chakula katika kata hiyo ni ya wastani kwa sababu wanazingatia elimu wanayotoa kila wakati na mpunga na mahindi yanazalishwa zaidi.

Amewataka wakulima kuacha tabia ya kuwapa mpunga wanawake wanaouza miili yao na wale wanaouza kwa lengo la kujipatia fedha kwa ajili ya familia zao wauze kichache na kuacha kingine kwa matumizi ya nyumbani.

Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Suzana Kayenge amesema kwa kulitambua hilo, wameweka utaratibu wa kupima VVU na Ukimwi kwa vijana wanaotaka kuoa na kuolewa lengo la kudhibiti maambukizi yasiendelee kuongezeka katika jamii na vifo kwa kundi hilo.

Susana, amesema anatarajia  kuanzisha msako  kwa kushirikiana na Kamati za Mtakuwa na serikali za vijiji na kuonya kuwa watakaobainika hawana makazi wataondolewa mara moja ili kutokomeza biashara hiyo ya ukahaba.