Makinda awafunda Yambesi na baraza lake MoCU

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 03:54 PM May 02 2024
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Anne Makinda (kushoto), akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, George Yambesi, alipozindua baraza la tatu jana.
Picha: Godfrey Mushi
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Anne Makinda (kushoto), akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, George Yambesi, alipozindua baraza la tatu jana.

SPIKA wa zamani wa Bunge, Anne Makinda, amesema ili kuepusha wakulima kuvamia ardhi ya Taasisi ya Elimu ya Ushirika na Biashara Kizumbi (KICoB) iliyoko Shinyanga na kuzusha ugomvi wa ardhi, Baraza la Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, linapaswa kufikiri kwa haraka namna ya kujilinda dhidi ya uvamizi wa wenyeji.

Aidha, amesema anategemea baraza hilo litasimamia uhuishaji wa mitaala na uanzishaji wa mitaala mipya ya mafunzo itakayoendana na mahitaji ya sasa na Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, Toleo la Mwaka 2023, inayotoa msisitizo kwenye ujuzi ili wahitimu kuajirika, kujiajiri na kuajiri wengine.

Makinda, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU, alikuwa akizungumza jana na jumuiya ya wanazuoni wakati uzinduzi wa Baraza la tatu la chuo hicho linaloundwa na wajumbe 17.

“Kampasi Yetu ya Kizumbi nimefika pale, eneo letu ni kubwa sana. Uzio unajengwa na majengo hapa (Moshi) lakini Kizumbi pako open (wazi). Mifugo na wenyeji wako pale, ingawa ni pazuri, lakini panahitaji pia hifadhi; kwa sababu itafika wakati watu wanaweza kuingia wakalima pale, wakaanza ugomvi wa ardhi.

“Yote haya yapo, lakini mimi naamini kabisa uwezo na nafasi ambayo mnayo katika chuo chetu, naomba mchukulie chuo hiki kama mtoto wenu kila mnapokwenda mnaweza kufikiria nini kinaweza kufanyika vizuri.

Zaidi alisema: “Vyuo sasa ni vya kisasa na viko vingi. Wingi wake si hoja, hoja ni baraza hili mnafanya nini kwa chuo hiki. Kama mlivyosikia, chuo hiki kina thamani kubwa sana, ndicho kilichojenga ushirika ndani ya nchi yetu yote na wataalam wote wanatokea hapa.

…Kwa hiyo dhamana yenu ya kujenga uchumi ni kubwa sana. Tena uchumi wa watu wadogo wadogo, sio uchumi wa mashirika makubwa. Ni watu wadogo wadogo katika nafasi zao.”

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Prof. Alfred Sife, alimweleza Makinda kuwa, MoCU kama taasisi inavyo vyombo vya kufanya maamuzi ngazi mbalimbali, akisisitiza chombo kikuu kabisa ni Baraza la Chuo ambalo hufanya kazi kwa kusaidiwa na kamati mbalimbali.

Alisema baraza hilo limeundwa kwa mujibu wa ibara ya 18 (1) ya Hati Idhini ya Chuo ya Mwaka 2015 na ukomo wa muda wa Mwenyekiti ni miaka minne na wajumbe ni miaka mitatu kwa mujibu wa kanuni ya 1 na 2 ya sehemu ya pili ya hati idhini ya chuo hiko.

Kabla ya uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa zamani Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa baraza hilo la MoCU, George Yambesi, alimweleza Makinda kuwa, idadi ya wanafunzi wanaohitimu chuoni hapo kila mwaka imefikia 3,500.

Kwa mujibu wa Yambesi, katika uhai wa baraza lililomaliza muda wake Machi mwaka huu, program za mafunzo zimefikia 39, huku udahili wa wanafunzi ukiendelea kuongezeka, ambapo kwa sasa chuo kinadahili takribani wanafunzi 9,000.