Miundombinu yawaliza Butimba

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:10 PM Apr 25 2024
Mvua zaharibu barabara.
PICHA: MAKTABA
Mvua zaharibu barabara.

WAKAZI wa Mtaa wa Kanyerere Kata ya Butimba Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza wamesema ukosefu wa miundombinu katika barabara yao umesababisha nyumba zao kukumbwa na mafuriko yanayosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Benedicto Mkwavi, mmoja wa wakazi hao ameliambia NIPASHE kuwa nyumba zao zimekuwa zikikumbwa na mafuriko mara kwa mara kutokana na ubovu wa barabara ya mtaa wao,  kukosa mtaro na kusababisha maisha yao kuwa hatarini.

Mkwawavi, amesema wamekuwa wakitumia  magunia  kunusuru nyumba zao kuharibiwa na kukumbwa na mafuriko. 

Ameushukuru uongozi wa Chama cha Democrasia  na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Nyamagana kwa kuwasaidia kuzibua baadhi ya mitaro, wameiomba serikali kuweka miuondombinu hiyo katika hali ya usafi.

Amesema wamekuwa wakiwasilisha malalamiko yao kwa uongozi wa kata hiyo,  lakini imeshindwa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.

 Zuwena Mapulu, amesema mvua hizo zimesababisha nyumba zao kuwa hatarini kuanguka, licha ya kuzingira, yamekuwa yakijaa hadi ndani.

Zuwena, amesema baadhi ya watoto wake wanaishi kwa ndugu zake kwa kuhofia mafuriko hayo kuwa yanaweza kuleta madhara kwao.

Viongozi wa CHADEMA wakiongozwa na Mhasibu Baraza la Wanawake (BAWACHA) Mkoa wa Mwanza, Veronica Kunju wakishirikiana  kuziba mifereji ya ya barabara hiyo ya mtaa, wamesema ubovu wa miuondombinu hiyo unasababisha baadhi ya watumiaji wa barabara kukosa huduma zinazostahili.

Marko Christian Mwenyekiti wa Baraza la Vijana  CHADEMA  (BAVICHA) Wilaya ya Nyamagana, amesema licha ya barabara ya mtaa huo kutengewa fedha  kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, miuondombinu ni mibovu na kuiomba serikali kulifuatilia suala hilo ili kuwarahisishia huduma ya usafri wananchi.