Nasibu apandishwa kizimbani tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 04:42 PM Apr 30 2024
Mtuhumiwa Nasibu Kisebengo (mwenye mfukio)  akipelekwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam kusoma mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin na cocine kinyume na sheria.
Picha: Grace Gurisha
Mtuhumiwa Nasibu Kisebengo (mwenye mfukio) akipelekwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam kusoma mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin na cocine kinyume na sheria.

MKAZI wa Mbezi jijini Dar es Salaam, Nasibu Kisebengo (44), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin na cocaine kinyume na sheria.

Akisoma hati ya mashtaka leo, Wakili wa Serikali Happy Mwakanyamale mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalloh amedai kuwa mshtakiwa huyo anatuhumiwa kwa mashtaka matatu ya kusafirisha dawa za kulevya ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Mwakanyamale amedai kuwa katika shtaka la kwanza, Kisebengo anatuhumiwa Februari 27, 2024 alikutwa eneo la Feri Tatavamba ndani ya Wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam akisafirisha dawa za kulevya aina ya heroin gramu 5.76 .

Amedai kuwa, katika shtaka la pili mshtakiwa alikutwa eneo hilo na tarehe hiyo akituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya cocaine gramu 0.82.

Wakili huyo ameendelea kudai kuwa, Februari 28,2024 mshtakiwa akiwa eneo la Mbezi Zone Makaranga ndani ya Wilaya ya Ubungo,Dar es Salaam alikutwa akisafirisha dawa za kulevya aina ya heroin gramu 20.96.

Baada ya mshtakiwa kusomewa mashtaka hayo alikana kuhusika na tuhuma hizo, Wakili Mwakanyamale amedai kuwa hakuna dhamana kutokana na mashtaka anayetuhumiwa nayo.

Pia, amedai kuwa upelelezi bado unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo na kuangalia hatua ya upelelezi ilipofikia. Hakimu Swalo ameharisha kesi hiyo hadi Mei 14,2024 kwa kutajwa