Rais Samia kufanyiwa kongamano la maombi

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 03:52 PM Apr 26 2024
Kiongozi wa kanisa hilo, Mwalimu Augustine Tengwa.
Picha: Christina Mwakangale
Kiongozi wa kanisa hilo, Mwalimu Augustine Tengwa.

KANISA la Uamsho na Matengenezo ya Kiroho, limeandaa kongamano la maombi maalum la kuliombea taifa na Rais Samia Suluhu Hassan, ili kudumisha amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu.

Kiongozi wa kanisa hilo, Mwalimu Augustine Tengwa, alitoa taarifa hiyo jana akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kongamano, litakalofanyika April 28, mwaka huu, viwanja vya Suma JKT, Mwenge, Dar es Salaam.

Alisema kongamano hilo litahusisha viongozi mbalimbali wa kiroho, waombaji na wananchi watakaomuombea  heri Rais Samia, kuendelea kuwa kiongozi bora kwa kuwaletea maendeleo na kudumisha amani na utulivu.

“Nilipata ufunuo Mungu akisema na mimi kumuombea Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, tumeandaa kongamano maalum kufanya maombi, nawakaribisha viongozi, waumini  kushiriki ibada hiyo kwa maslahi ya taifa letu,” alisema Tengwa.

Alisema ameandaa ajenda mbalimbali kwa ajili ya kuziombea ikiwamo, kumuombea Rais Samia, Mungu, kumpa ustahimilivu na uvumilivu kuwatumikia wananchi.

“Mungu amenisemesha  kuanzia huu mwezi wa nne, tutakuwa na maombi  mfululizo ya  kumuombea Rais na taifa  hadi muda wa uchaguzi, ili ufanyike kwa amani,” alisema.

Baadhi ya viongozi wa dini walioshiriki kutoa taarifa hiyo, walisema wapo tayari kuliombea taifa la Tanzania, ambalo kwa Afrika limekuwa la mfano, kwa  wananchi wake kuwa watulivu wanaodumisha amani.