Samia aagiza mambo 5 wizara, Tume ya Ulinzi Taarifa Binafsi

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:59 AM Apr 04 2024
Rais Samia Suluhu Hassan.
PICHA: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan, amezindua Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na kutoa maelekezo matano kwa wizara na taasisi za umma, huku akitoa miezi tisa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) iwe imesomana.

Kadhalika, ameitaka Tume hiyo kuhakikisha taasisi zote za umma na binafsi zinasajiliwa na kutekeleza Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kabla ya mwezi Desemba, mwaka huu.

Rais Samia ametoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa binafsi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Pili, taasisi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi zihakikishe zinazingatia matakwa ya sheria ya ulinzi binafsi na tume itoe elimu kusisitiza wajibu wa taasisi hizo.

“Tatu, maofisa Tume mna kazi kubwa ninataka muifanye kwa weledi na ubora zaidi muwe wadhibiti, lakini pia wawezeshaji ili watoa huduma mbalimbali waridhike na utunzaji wa haki binafsi nchini.

Pia, ametaka jitihada zilizofanywa kwa muda mrefu, wizara na Tume wakazitimize.

Jambo la nne, amelielekeza kwa Waziri Nape kwa upande wa sera wafuatilie kwa karibu kazi za Tume ili malalamiko yanayoibuliwa yashughulikiwe kwa haki.

Ameiagiza wizara hiyo impelekee taarifa ya utekelezaji mara mbili kwa mwaka ili kujua mwenendo wake.

“Mkurugenzi Mkuu wa Tume na Mwenyekiti wote ni polisi, tunategemea kuona utendaji haki wa kesi na uendeshaji wake yanakwenda kama mafunzo ya kipolisi yanavyosema,” amesema.

Jambo la tano, Rais Samia amelielekeza kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, kusimamia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yote isomane.

Amesema kuna taasisi muhimu zipo maeneo mbalimbali, akitoa mfano, NIDA, E-Ga na Tume hiyo, akitaka ziwe na mratibu asiyefungamana na upande wowote.

Kuhusu suala la taarifa binafsi, Rais Samia alisema miaka ya nyuma duniani kuna visa vilitokea kutokana na kuvuja taarifa.

Pia, amesema vitendo vibaya vilivyofanywa na watu na vikundi visivyo vyema, kudukua mifumo ya taasisi zinazokusanya taarifa binafsi yakionesha ukiukwaji wa haki za watu.

Hayo yote amesema yalisababishwa na udhibiti hafifu wa mifumo ya ukusanyaji, utunzaji na utumiaji wa taarifa binafsi katika taasisi mbalimbali.

“Katika kukabiliana na haya yote ndio maana tupo hapa leo kuzindua Tume ya Ulinzi Binafsi. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka bayana kulindwa kwa taarifa binafsi za watu au haki za binadamu.

Pia, amesema Ibara ya 16(2) ya Katiba imezitaka mamlaka za nchi kuweka utaratibu wa kisheria wa namna ya kulinda haki ya faragha na Ibara ya 12 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu mwaka 1948, inayataka mataifa kuweka utaratibu kuhakikisha mtu yeyote haingiliwi faragha yake.

Kikanda suala la ulinzi wa haki ya faragha limepewa kipaumbele katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na miongozo mbalimbali.

Kadhalika amesema Umoja wa Afrika kupitia Mkataba wa Malawi wa mwaka 2014, unasisitiza ulinzi wa faragha.

“Mwaka 2015 nchi yetu imeunda sheria mbili kati ya hizi tatu, ya Makosa ya Mtandao na Miamala ya fedha. Sheria ya ulinzi binafsi tumeshafanya hivyo na leo (jana) tunazindua Tume,” amesema.

Amesema kuundwa kwa sheria hiyo na uzinduzi wa Tume sio tu wametekeleza matakwa ya Katiba, bali ahadi ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kukamilisha wajibu wao wa kikanda na kimataifa na kwamba, hawana deni wameshakamilisha.

Rais Samia amekumbusha kila mtu ana utashi na anastahili staha, hivyo zipo baadhi ya taarifa asingependa zijulikane kwa kila mtu.

“Na kwa kweli ingekuwa taarifa zetu zote zipo wazi na watu wanazijua tusingetazamana usoni au hii dunia ingekuwa dunia ya aina nyingine, hakuna faragha wala staha. Tumekuja na sheria hii ili kutunza utu wa mwanadamu,” amesema.

Rais Samia amesema zipo baadhi ya taarifa ambazo zinaweza kutumika kuhujumu jamii nzima na wakati mwingine kusababisha unyanyapaa na nyingine, zinaweza kuleta vurugu au vita na mauaji.

 “Sasa hii haikuwa sawa. Licha ya taarifa binafsi kutumika kwa hujuma, lakini pia ni biashara kubwa kwa kampuni mbalimbali za kimtandao, hivyo hatuna budi kulindana ili zisitumike.”

Amesema serikali imelazimika kuweka utaratibu wa kisera na kisheria ili kulinda taarifa binafsi za Watanzania zinazokusanywa na kuchakatwa, kuhifadhiwa na wakati mwingine kusafirishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

"Leo tunapozindua Tume hii, Tume itambue ina kazi nzito na ni muhimu kwa maisha ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. 

“Usalama wetu kiuchumi, kisiasa na kijamii upo mikononi mwenu Mwenyekiti wa Tume na Mkurugenzi wa Tume na wajumbe na wafanyakazi wa Tume maisha yetu yapo mikononi mwenu, heshima zetu zipo mikononi mwenu,” amesema.

 Amesema Tume hiyo inakwenda kuvutia mitaji na mambo mengine ya kukuza uchumi wa kidijitali.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema tukio la uzinduzi wa Tume limeiweka Tanzania katika orodha ya nchi za wastaarabu duniani wanaoheshimu utawala wa sheria, ubinadamu na faragha za watu na kuchangia katika jitihada za dunia kufanya ulimwengu wa mtandao kuwa salama.