Sera ya elimu bila malipo kizungumkuti vijijini

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 03:24 PM Apr 25 2024
Diwani wa Kata ya Mlangali ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Hamisi Kayombo.
PICHA: MAKTABA
Diwani wa Kata ya Mlangali ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Hamisi Kayombo.

SERIKALI mkoani hapa imeombwa kwenda maeneo ya vijijini kwa wananchi ili kutoa elimu juu ya sera ya elimu bila ya malipo kwa sababu inatajwa kupokelewa tofauti.

Ombi hilo limetolewa na Diwani wa Kata ya Mlangali ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Hamisi Kayombo katika kikao cha wadau wa elimu na utoaji tuzo za elimu kilichofanyika mkoani hapa.

Kayombo, amesema sababu kubwa inayofanya shule kushindwa kufaulisha si walimu bali ni sera ya elimu bila ya malipo kupokelewa tofauti hasa maeneo ya vijijini.

“Mheshimiwa Mwenyekiti sera ya elimu bila ya malipo baadhi ya maeneo, elimu haijawafikia vizuri wazazi wanaamini kwamba elimu bila ya malipo kila kitu serikali inatakiwa walipe, wanavyokuja walimu na changamoto za mahitaji ya wanafunzi wazazi wanasema sera ya elimu bila ya malipo tumeambiwa kuanzia mitihani, walimu hapa hakuna michango mtoto asome bure,” amesema na kuongeza kuwa:

“Kuna maeneo tumezidiwa walimu hawapo wa kutosha tunapowaambia wazazi tuajiri walimu wa kujitolea, mzazi ananijibu mimi nimeambiwa elimu bure,” 

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka, amesema ili mtoto aweze kufanya vizuri katika masomo yake ni vizuri kukawa na muunganiko wa moja kwa moja kati ya mzazi na mwalimu.

“Lazima tuheshimu walimu, mwalimu ni mtu wa msingi katika maisha ya mtoto na ili kuwekeza katika elimu ipo haja ya kuwaheshimu walimu,” amesema Mtaka.

Awali Mratibu wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Joel Mhoja, amesema bado kuna tatizo kubwa la wanafunzi kutofaulu somo la Hisabati na Kiingereza nchini.

“Imefikia hatua Baraza la Mitihani la Taifa kuindikia Wizara ya Elimu na ofisi ya TAMISEMI kwamba kuwepo umakini kwenye ufundishaji wa haya masomo hali sio nzuri,” amesema Mhoja.