Serikali na mikakati kuimarisha sekta madini

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 10:04 AM May 01 2024
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
PICHA: MAKTABA
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

MADINI ya dhahabu yanayozalishwa nchini yametajwa kupanda bei kwa zaidi ya asilimia 86 kwa kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Machi 2024 huku Tanzania ikitajwa kuwa na zaidi ya tani 45 ya madini hayo.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25 na kuomba kuidhinishiwa Sh. bilioni 231.9 kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo.

Mavunde  amesema kwa kipindi hicho, bei ya madini ya dhahabu kwa wakia ilipanda hadi kufikia wastani wa Dola za Marekani 2,138.01 ikilinganishwa na bei ya wastani wa Dola za Marekani 1,854.54 katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023.

Amesema kuongezeka kwa bei ya dhahabu kunatokana na sababu mbalimbali ikiwamo mahitaji makubwa ya madini hayo duniani.

“Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba nchi yetu ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na madini mkakati ambayo uhitaji wake ni mkubwa kwenye nishati safi na salama na teknolojia nyingine za kisasa duniani.”

MKAKATI MADINI KUINUFAISHA

Kuhusu mikakati mbalimbali katika sekta ya madini inayolenga kuyafanya madini yalinufaishe taifa, Mavunde alisema wizara imeandaa mkakati muhimu wa uendelezaji wa madini muhimu na madini mkakati nchini.

Amesema mkakati huo unalenga kuhakikisha madini hayo yanaongezwa thamani ikiwamo kuzalisha bidhaa zinazohitajika katika soko la betri za magari ya umeme na kuongeza manufaa kwa nchi ikiwamo mapato ya serikali na ajira kwa Watanzania.

Vilevile,  amesema ili kuongeza manufaa yatokanayo na madini muhimu na madini mkakati, kwa mara ya kwanza kitajengwa kiwanda kikubwa na cha kisasa cha usafishaji na uongezaji thamani cha Multi Metals Processing Facility katika eneo maalumu la ukanda wa kiuchumi la Buzwagi Special Economic Zone, Wilaya ya Kahama.

Pia, wizara imeandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Madini Sura ya 123 ambayo yaliwasilishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa 14 wa Bunge kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na. 4 ya Mwaka 2024, ili kuweka mazingira mazuri katika sekta ya madini.

Amesema katika kuhakikisha kuwa mchango wa Sekta ya Madini katika kuliingizia taifa fedha za kigeni unaongezeka, wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa matakwa ya kifungu cha 10 cha Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusu Umiliki wa Utajiri Asilia na Maliasilia za Nchi, Sura ya 449 kinachoweka sharti la mapato yatokanayo na uvunaji wa maliasilia za nchi ikiwemo madini kuwekwa katika taasisi za fedha zilizopo nchini.

Itaendelea kushirikiana na mamlaka nyingine za serikali ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhakikisha malipo ya mauzo ya madini yaliyofanyika nje ya nchi yanarejeshwa nchini.

UWEKEZAJI SEKTA MADINI

Wizara inatarajia kufanya uwekezaji utakaojikita kupata taarifa za jiolojia kwa kufanya utafiti wa kina kupitia “Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri”.

Vilevile, kuandaa Programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) kwa ajili ya kuwainua wachimbaji wanawake na vijana, kuongeza tija kwenye shughuli za uongezaji thamani madini kupitia utoaji wa vifaa vya uongezaji thamani madini kwa wahitimu wa TGC.

Kupitia GST itaendelea kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kutambua tabia za miamba na kurahisisha utafiti nyingine za jiosayansi zenye kuwezesha kubaini aina mbalimbali za madini yapatikanayo nchini.

LESENI KUFUTWA

Waziri Mavunde  amesema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, leseni 96 za utafutaji wa madini, 11 za uchimbaji wa kati na mbili za uyeyushaji zilipewa hati za makosa kutokana na kutozingatia masharti ya leseni ikiwa ni pamoja na kutolipa ada za mwaka na kutoendeleza maeneo ya leseni.

Amesema, leseni tisa za utafutaji madini na mbili za uchimbaji wa kati zilifutwa baada ya wamiliki wake kushindwa kurekebisha makosa.

Aidha,  amesema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, Tume ya Madini ilitoa leseni 10,067 ikilinganishwa na lengo la kutoa leseni 6,921.