Serikali yabanwa mikopo ‘kausha damu’

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 02:14 PM Apr 25 2024
Mikopo kausha damu.
PICHA: MAKTABA
Mikopo kausha damu.

SAKATA la mikopo inayolalamikiwa, maarufu kama ‘kausha damu’, limeendelea kuibuka bungeni huku wabunge wakihoji mikakati ya serikali wa kuzibana taasisi zinazotoa mikopo kwa riba kubwa hali inayosababisha magonjwa ya afya ya akili na uvunjifu wa ndoa.

Aidha, Spika wa Bunge, Dk.Tulia Ackson ameiagiza Wizara ya Fedha kutafuta uhakika kama kuna kampuni za simu nchini zinatoa mikopo ya aina hiyo. 

Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Felista Njau, amehoji mkakati wa serikali wa kukomesha mikopo ya kausha damu ili kunusuru wananchi ambao wamekuwa wakipata matatizo ya afya ya akili na ndoa nyingi kuvunjika.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo ametaka kujua kuna mkakati gani kufuatilia na kuchukua hatua kwa taasisi za fedha zinatoa mikopo yenye riba kubwa kinyume cha muongozo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Pia Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Shally Raymond, amesema pamoja na sheria ya BoT ya mwaka 2018 na kanuni za 2019 lakini mikoa zaidi ya 17 ukiwamo wa Kilimanjaro hasa wilaya ya Moshi vijijini imekuwa ikitolewa mikopo kausha dam una kuhoji serikali inatoa kauli gani.

“Kampuni za simu zimekuwa zikitoa mikopo haraka bila kujaza fomu na vijana na wanawake wajasirimali wa Kilimanjaro wamekuwa wakichangamkia fursa hiyo lini serikali italazimisha kampuni hizo kutoa elimu,” amesema.

Kutokana na kauli hiyo, Spika Tulia amesema hana uhakika kama kampuni za simu ambazo zimesajiliwa zinatoa mikopo kausha damu kama taasisi nyingine ambazo hazijasajiliwa.

“Naibu Waziri wa Fedha nakupa muda baada ya kipindi cha maswali katafute habari za uhakika hapo nje kwa kampuni za simu kama zinatoa mikopo kausha damu,” amesema .

Awali, akijibu maswali ya wabunge hayo, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, ameelekeza taasisi zinazotoa mikopo hiyo kuacha mara moja na serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo.

Pia ameagiza BOT kufuatilia taasisi zinazoenda kinyume na sheria hiyo, na serikali haitakuwa na muhari kwa taasisi zinazokiuka sheria hizo na kanuni hizo , ikiwamo ya kufutiwa leseni ya kutoa huduma hiyo.

Amesisitiza serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera, kiutawala na kisheria ili kudhibiti tabia ya baadhi ya taasisi za fedha kutoa mikopo kinyume na miongozo iliyopo.

“Hatua hizi ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kusimamia ukwasi katika mfumo wa kibenki ili kuendana na mahitaji halisi ya kiuchumi na kuweka mazingira rafiki ya utoaji mikopo,” amesema.

Amesema wataendelea kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya fedha ili kumsaidia mwananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu fursa za mikopo zilizopo, viwango vya riba na athari zake, vigezo vya kuzingatia na umuhimu wa kurejesha mikopo.

Pia amesema serikali itaendelea kufanya kaguzi, ufuatiliaji na tathmini ya uzingatiaji wa sera, sheria na miongozo iliyopo ili kuboresha na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wale wanaobainika kukiuka taratibu.