Serikali yapokea ushauri wa TUCTA kuiwezesha CMA

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 11:11 AM May 02 2024
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.
PICHA: MAKTABA
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.

SERIKALI imesema imepokea ushauri wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), la kuiwezesha Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kuboresha huduma zake.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango alipojibu hoja ya hotuba iliyowasilishwa na shirikisho hilo katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yaliyofanyika mkoani Arusha kitaifa.

Amesema serikali kwa kutambua umuhimu wa CMA na ushauri wa TUCTA itaiwezesha kupata vitendea kazi pamoja na kuongeza nguvu kazi ili kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kuwapatia magari kwaajili ya usafiri ili kuwafuata walalamikaji wa migogoro ya kikazi walioko mbali na Ofisi za Tume.

Katibu Mkuu wa TUCTA, Henry Mkunda wakati akiwasilisha hotuba yake alisema kuiwezesha Tume hiyo kutasaidia kuimarisha ufanisi na wafanyakazi kupata haki zao hasa walioko Katikati ngazi ya Wilaya ambako huduma hazipatikani.

Rais TUCTA, amesema, CMA itasaidia kutatua changamoto ya migogoro ya wafanyakazi katika mikoa na ngazi ya wilaya ambako kumeonekana kukosa huduma hiyo hivyo kuwanyima wananchi haki yao.

CMA ni taasisi huru inayoshughulika na utatuzi wa migogoro ya Kikazi Tanzania bara, baina ya Mwajiri, mwajiriwa pamoja na vyama vya wafanyakazi.