TFS yatoa milioni 20, msaada kwa waathirika wa mafuriko Rufiji, Kibiti

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:59 PM Apr 25 2024
Mkuu  wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, akipokea mfano wa hundi ya shilingi milioni 20 kutoka kwa Afisa Uhusiano wa TFS Johari Kachwamba.
Picha: Julieth Mkireri
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, akipokea mfano wa hundi ya shilingi milioni 20 kutoka kwa Afisa Uhusiano wa TFS Johari Kachwamba.

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amepokea hundi ya sh. milioni 20 kutoka kwa Wakala wa Huduma za Mistu Tanzania (TFS) kwa ajili ya Waathirika wa mafuriko katika Wilaya ya Rufiji na Kibiti.

Kunenge, ameishukuru taasisi hiyo kwa kuungana na wadau wengine kuwasaidia waathirika wa mafuriko ambao nyumba zao zimezingirwa na maji huku mazao yao yakiharibika.

Mkuu huyo wa mkoa pia ameshukuru TFS kwa kutoa eneo la viwanja 600 vya makazi kwa ajili ya waathirika wa mafuriko Rufiji ambao nyumba zao zimezingirwa na maji.

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo, Afisa Uhusiano wa TFS Johari Kachwamba amesema wametoa msaada huo kutokana na kutambua mchango wa wananchi hao kwenye uhifadhi kwani katika Wilaya ya Rufiji wana misitu zaidi ya 10 yenyewe hekta zaidi ya 32,000.

Amesema katika kusaidiana na Serikali katika kutatua changamoto za mafuriko kwa wilaya hizo wametoa msaada huo ambao wanatarajia utakwenda kusaidia waathirika hao.

Wilaya ya Rufiji hadi sasa ni kata 12 kati ya 13 zilizoathirika na mafuriko huku Wilaya ya Kibiti wananchi 36,900 nyumba zao zikiathiriwa na maji.