Waathirika mafuriko Lindi waomba maeneo mbadala

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:59 AM Apr 22 2024
Maafa yaliyotokana na mvua.
PICHAA: MAKTABA
Maafa yaliyotokana na mvua.

WAATHIRIKA wa mafuriko Mitaa ya Mtange, Kata za Jamhuri na Rupiani Manispaa ya Lindi, wameiomba serikali kuwapatia maeneo mbadala ya kuishi ili kunusuru maisha yao.

Wananchi hao walitoa ombi hilo kwa wenyeviti wa mitaa yao, Amiri Rajabu na Hatibu Mohamedi walipokuwa wanapokea msaada wa vyakula vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni nne kutoka Kamati ya Maafa ya Manispaa ya Lindi.

Msaada huo ni pamoja na unga wa mahindi, maharage, mafuta ya kupikia, sabuni na chumvi.

Wenyeviti wa mitaa hiyo wamesema kutokana na maafa waliyapata mwaka huu, wapo tayari kubadilisha makazi kutoka maeneo ya mabondeni ambayo sio rafiki kwa salama wa maisha yao na kwenda kuhamia maeneo yenye miinuko. 

“Tunachokuomba mkurugenzi tumia wataalamu wako idara ya aridhi kutupimia viwanja vya bei nafuu maeneo yaliyoinuka tumechoshwa na mateso haya,” wamesema Rajabu na Hatibu.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Juma Mnwele, ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya maafa akipokea ombi hilo, amehaidi kulifanyia kazi, huku akiwataka wanaoishi mabondeni kuchukua tahadhari ya kuishi kwenye maeneo yenye miinuko.

Amesema serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wananchi wake, huku akiwasisitiza kuchukua taadhari ya kuwalinda watoto, wazee wasiojiweza na wenye ualemavu kuwaangalia mara kwa mara mvua zinazopeleka maji ndani ya nyumba zao.