Maofisa waonywa kuinglilia mifumo malipo

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe
Published at 06:11 AM May 04 2024

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, ameonya baadhi ya maofisa utumishi wanaoingia katika mfumo shirikishi wa taarifa za kiutumishi na mishahara (New HCMIS) kusimamisha mishahara na makato ya mishahara ya wenzao bila kufuata taratibu zilizowekwa kwa lengo la kuwakomoa.

Akizungumza jana jijini hapa katika ufunguzi wa  mkutano wa 11 wa mwaka wa Jumuiya ya  Utawala wa Umma kwa Kanda  ya Tanzania, Simbachawene alisema maofisa utumishi wameaminiwa  na kupewa dhamana ya kuingia katika mifumo hiyo, hivyo wanapaswa kutumia dhamana waliyopewa kwa uadilifu mkubwa, ili kuondoa malalamiko yanayoonesha uvunjifu wa maadili na ukiukwaji wa taratibu za kiutendaji. 

Pia alionya baadhi ya maofisa wenye tabia ya kutoa taarifa ambazo wanakutana nazo katika mifumo hiyo kwa watu wasiohusika. 

"Nyie mmeaminiwa vizuri mkabadilika kwa kusimamia maadili na miiko ya kazi zenu, kwa kujiepusha kutoa taarifa za mifumo kwa watu wasio wahusika," alisema. 

Kwa mujibu wa Simbachawene, ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma; na kuongeza uwajibikaji na uwazi wa watoa huduma na wapokea huduma, kuanzia tarehe 2 Aprili mwaka 2024, ilielekezwa uhamisho wa watumishi ushughulikiwe kupitia mfumo wa e-uhamisho.  

"Ni dhahiri kuwa ushughulikiaji wa uhamisho kupitia mfumo huo, utasaidia kuondokana na changamoto za udanganyifu na upendeleo unaoweza kujitokeza, kutokana na mahusiano kati ya mtoa huduma na mpokea huduma,"alisema.  

OR-MUUUB kama msimamizi wa Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma, imekuwa ikipokea mrejesho juu ya utendaji wao. 

"Baadhi ya maeneo yanayolalamikiwa ni pamoja ucheleweshaji wa upatikanaji wa stahiki za watumishi, kutoa lugha  zisizofaa kwa watumishi na wateja, na kushindwa kusimamia maadili ya watumishi ipasavyo,"alisema. 

Aidha, alisema waache kushughulikia hoja za watumishi ambazo zinapaswa kumalizwa katika ngazi ya waajiri na badala yake kuacha watumishi kutafuta suluhisho kwa viongozi wa kisera na viongozi wakuu wa kitaifa si sahihi. 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wataalam Tawi la Tanzania (AAPAM Chapter- Tanzania), Leila Mavika, alisema mkutano huo ni sehemu ya kujegeana uzoefu na kaulimbiu yake ni  ‘Usimamizi wa Utendaji Kazi Katika Utoaji wa Huduma: Nafasi ya TEHAMA Katika Kuimarisha Utendaji Kazi Katika Utumishi wa Umma".