Wabunge wataka maji kwa uwekezaji

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 02:40 PM Apr 25 2024
Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi.
PICHA: MAKTABA
Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi.

Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji imatakiwa kuweka mkakati wa kutumia kikamilifu maji yakiwamo ya Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa uwekezaji hasa kilimo cha umwagiliaji ili kusaidia kuongeza pato la taifa.

Ushauri huo umetolewa na wabunge kwa nyakati tofauti wakati wa uchangiaji wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo kwa mwaka 2024/25.

Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, amesema uwekezaji kupitia maji kwa zaidi ya miaka 60 umeendelea kuwa chini licha ya taifa kuwa na rasilimali nyingi za maji yakiwamo ya maziwa ya Victoria na Tanganyika.

Amesema mpaka sasa uwekezaji katika umwagiliaji nchini ni asilimia mbili tu licha ya upatikanaji maji katika vyanzo hivyo ambayo yakivunwa yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika uwekezaji.

“Ni vyema sasa tukawekeza na kuweka mipango mirefu kwenye Tume ya Umwagiliaji na kuiwezesha kwa mpango wa miaka mitano mitano ihakikishe inaongeza sehemu ya umwagiliaji. Lazima  tuangalie uwezekano wa kutumia maji katika maziwa yetu  kwenye kilimo na ufugaji.

“Kwa hiyo hapa Waziri (Prof.) Kitila (Mkumbo) kuna shughuli kubwa ya kwenda kufanya kwa sababu hili tatizo kubwa la ajira tunalolizungumza ni kutokana na kuwa hatujaweka mipango yetu vizuri kwani tukiimarisha huku kwenye kilimo na ardhi hatutaona Mtanzania yeyote akizunguka na bahasha,” amesema Shangazi.

Mbunge wa Ukerewe (CCM), Joseph Mkundi amesema katika uwekezaji bado Tanzania haijaweza kutumia vyema rasilimali maji hususani kwa Ziwa Victoria katika kilimo cha kisasa cha umwagiliaji.

“Sasa ni vyema tuone namna sahihi ya kuwekeza zaidi katika kilimo ambacho tumeona kinaajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania ili kujenga uchumi wetu kama taifa pamoja na uchumi wa mtu mmoja mmoja,” amesema Mkundi.

Amesema pamoja na jitihada zinazoendelea kufanyika, bado serikali haijatumia ipasavyo rasilimali zilizopo likiwamo Ziwa Victoria na kuwa endapo ziwa hilo pamoja na mengine yatatumika ipasavyo, taifa litafikia mapinduzi makubwa ya kiuchumi ikiwemo kuzalisha ajira nyingi kwa Watanzania hususan vijana.

“Eneo kama Ukerewe limezungukwa na maji na yapo maeneo mengi ambayo tunaweza kuwekeza kilimo cha umwagiliaji, nishauri tufanye uwekezaji huko ili kuzitumia ipasavyo rasilimali zetu,” amesema Mkundi.

CHANGAMOTO WAWEKEZAJI

Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Agnesta Kaiza, amesema suala la ubovu wa miundombinu nchini bado ni tatizo kwa wawekezaji hali inayopunguza kasi ya uwekezaji nchini.

Ametaja miundombinu hiyo kuwa ni pamoja na barabra, maji na umeme ambao si toshelevu kwa viwanda.

“Mfano katika eneo la Makondani uwekezaji uliopo ni mkubwa kulinganisha umeme uliopo ambao ni mdogo unaosababisha kukwama kwa shuguhuli za uendeshaji viwanda. Si  umeme tu bali hata barabara ni mbovu pamoja na upatikanaji hafifu wa maji, hivyo serikali ifanyie kazi suala hili ili kuboresha mazingira ya uwekezaji,” amesema Kaiza.

Aidha, ametaja tatizo la sheria za uwekezaji nchini kutokusomana na sheria nyingine hali inayosababisha usumbufu kwa wawekezaji wanaoingia nchini kuwekeza kwa kufuata sheria za uwekezaji lakini wanakutana na vikwazo katika sheria nyingine.