Wabunge wataka utafiti kuinusuru Shule ya Sheria

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 09:54 AM May 01 2024
Shule ya sheria.
PICHA: MAKTABA
Shule ya sheria.

WABUNGE wameitaka serikali kufanya utafiti wa kina kuhusu idadi kubwa ya wanafunzi wa Shule ya Sheria Tanzania (LST) kushindwa mitihani na kubaini mzizi wa tatizo hilo na kuja na suluhisho la kudumu ikiwa ni pamoja na kuweka mchujo wa wanafunzi kabla ya kuanza masomo hayo.

Mbunge wa Jimbo la Manyoni (CCM), Dk. Pius Chaya, amesema hali ya kufeli kwa wanafunzi wanaosoma shule ya sheria nchini imekuwa ya mwendelezo kila mwaka na kuonesha upungufu katika maeneo mbalimbali yanayotakiwa kufanyiwa kazi ili kurejesha heshima yake.

Ametaja upungufu huo kuwa ni pamoja na utofauti wa vyuo vinavyotoa shahada ya sheria nchini kutokana na uwekezaji pamoja na utofauti katika ufundishaji hali inayosababisha baadhi ya wahitimu wa vyuo fulani kufaulu mitihani hiyo huku wengine wakishindwa.

Aidha, ameshauri serikali kuwaka mchujo kwa wanafunzi wanaotoka vyuoni kwa kufanya mtihani utakaowaruhusu kuendelea na masomo huku watakaoshindwa mtihani huo waendelee na shughuli nyingine zinazohusiana na taaluma hiyo kuliko kuendelea kupoteza muda wao.

Dk. Chaya ametoa mapendekezo kuwa serikali ije na mkakati wa kubadilisha mtaala wake ili uegemee zaidi katika utolewaji wa elimu kwa vitendo zaidi ya kusoma kama walivyokuwa wakisoma vyuoni.

Amesema haja ya serikali kutumia wataalamu waliobobea katika masuala ya sheria kwa vitendo kuliko wale waliobobea kwenye taaluma ya ufundishaji pekee kwani shule hiyo ipo kwa ajili ya kufundisha sheria kwa vitendo zaidi.

Mbunge wa Viti Maalum, Salome Makamba, amesema wanafunzi wanaoingia katika shule ya sheria wanakuwa na ufaulu wa juu, lakini cha kushangaza wanaofaulu ni wachache.

Amesema wapo wanaosoma katika shule hiyo na kufeli masomo yao kisha kuachana na masomo hayo na kuendelea na shahada ya uzamili na kupata ufaulu wa juu kwa masomo hayo hayo.

“Naomba kwenye suala hili tusifanye utafiti wa kisiasa bali tufanye utafiti wa kitaalamu kwa sababu hakuna ‘kilaza’ (mjinga) anayesoma sheria kwenye nchi hii kwani kila anayesoma sheria ni yule aliyepata wastani wa juu kuanzia kidato cha nne hadi chuo kikuu,” amesisitiza Salome.

Akijibu hoja hizo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Pindi Chana, amesema tayari mapitio ya mtaala yameanza kufanyika na kuwa mtaala mpya utaanza kutumika ifikapo Julai 2024.

Dk. Chana  amesema shule hiyo ya sheria imewekwa kwa mujibu wa sheria na kuwa kila mwanafunzi anayeanza masomo hapo lazima awe amekidhi vigezo ikiwa ni pamoja na kuwa na shahada ya sheria (LLB) hiyo kigezo hicho kinatosha kuendelea na masomo bila kuwekewa mtihani wa kuchujwa.

“Law School of Tanzania imekuwa ikiwatumia wataalamu wabobezi na kwa sasa ina kanzi data yenye wabobezi zaidi ya 80 kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya kisheria wakiwamo majaji, mawakili wa serikali na mawakili wa kijitegemea hivyo mapendekezo mengine yaliyotolewa yataendelea kufanyiwa kazi,”  amesema Dk. Chana.