'Wadudu' wala kiapo, Makonda awataka wasijihusishe na uhalifu

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 12:25 PM May 02 2024
Vijana zaidi ya 223  wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za sanaa maarufu kama 'Wadudu' wakila kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda.
Picha: Mpigapicha Wetu
Vijana zaidi ya 223 wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za sanaa maarufu kama 'Wadudu' wakila kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amekutana na vijana zaidi ya 223 wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za sanaa maarufu kama 'Wadudu' na kuwataka kuwa walinzi na mabalozi wazuri wa kutangaza mazuri ya mkoa wao wa Arusha na kutojihusisha na uhalifu kwenye Jamii.

Makonda amekutana na vijana hao ofisini kwake leo Mjini Arusha ikiwa ni muendelezo wa kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii katika kuwaeleza maono yake na kuwashirikisha ili kushirikiana na mkoa katika kujiletea maendeleo.

Aidha, Makonda amewataka vijana hao kutumia vipaji vyao vizuri ili viwasaidia kuingiza kipato, akiwataka kumuheshimisha kama ambavyo ameonyesha thamani kwao tofauti na vile ambavyo wengi walifikiri.

Aliwashauru vijana hao kumtanguliza Mungu kwenye maisha yao kuwa na nidhamu na kuchagua uongozi ili kufanikisha kupatiwa mahitaji ambayo tayari walikwisha kuyawasilisha kwake kwenye kikao cha awali ambacho walikutana pamoja.

Vijana hao wamemuahidi Makonda kutekeleza maelekezo na maagizo yake na watampatia ushirikiano kwenye utekelezaji wa maono yake katika Mkoa wa Arusha.