Wahifadhiwa kituo cha afya baada ya nyumba kuzingirwa na maji ya Ziwa Victoria

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 03:48 PM May 05 2024
Moja ya nyumba zilizozingirwa na maji ya Ziwa Victoria.
Picha: Mpigapicha Wetu
Moja ya nyumba zilizozingirwa na maji ya Ziwa Victoria.

MVUA inayoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini, imesababishamaji ziwa Victoria kuongezeka na kuingia katika nyumba katika kisiwa cha Rukuba kilichopo Kata ya Etaro Musoma Vijijini mkoani Mara.

Kaya tano kwa sasa zimelazimika kuhamia kituo cha afya kilichopo kisiwani hapo kutokana na kuvamiwa na maji ya ziwa hilo, huku Kaya nyingine 32 zikiwa katika hatari ya kukumbwa na maji hayo.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo amesema, maji yameongezeka kiasi Cha mita 1.65.

"Nimewasiliana na wataalam wa Bonde la Ziwa Victoria huko Mwanza, amekiri kuongezeka Kwa kiasi hicho cha maji na kutoa ushauri," amesema Prof.Muhongo.

Ametaja ushauri wa wataalam hao kuwa ni watu wanaoishi karibu na ufukwe wa ziwa kukubali ushauri watakaopewa na viongozi ili kuepuka mafuriko au ongezeko la maji katika ziwa hilo.

"Lakini pia, wananchi wanatakiwa kufuatilia utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na wataalam wa hali ya hewa nchini," 

Aidha, amewakariri baadhi ya waathirika wa kisiwani humo wakisema maji yamewafuata kwa takriban mita 30 hadi 40 hadi katika makazi yao.

 "Ziwa Victoria lenye kawaida ya ujazo wa maji wa takriban kilomita za ujazo 2,424 (2,424 cubic kilometres), kwa sasa maji yaongezeka sana, tuchukue tahadhari kubwa,"amesema.