Wakazi 374 kulipwa kupisha hifadhi Bwawa la Mindu

By Christina Haule , Nipashe
Published at 11:49 AM Apr 30 2024
Wakazi 374 kulipwa fidia kupisha hifadhi Bwawa la Mindu.
PICHA: MAKTABA
Wakazi 374 kulipwa fidia kupisha hifadhi Bwawa la Mindu.

ZAIDI ya kaya 374 za wakazi wa Kata ya Mindu, Manispaa ya Morogoro, wanatarajia kulipwa fidia na kupelekwa eneo la Suluhu New city, wilayani Mvomero mkoani hapa walikuwa ndani ya mita 500 Bwawa la Mindu ili kupisha hifadhi.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mikoroshini, Kata ya Mindu, Shomari Mwinyimvua, amesema hayo kwenye kikao cha mrejesho wa serikali kwa wananchi kuhusu mgogoro wa muda mrefu wa uvamizi wa eneo la pembezoni mwa Bwawa la Mindu na kuishukuru serikali kwa kuamua kuwalipa fidia wakazi wa maeneo hayo huku pamoja na fidia hizo ikiwapa viwanja wakazi walio ndani ya mita 500 ya bwawa hilo.

Mwinyimvua  amesema changamoto hiyo iliwakumba ndani ya miaka mingi wakitishiwa kuondolewa kwenye viwanja vyao bila hata kulipwa fidia, lakini baadae serikali ikaamua kuwalipa fidia wanaokaa upande wa juu ya bwawa kuvuka barabara huku ikiwataka kutojenga vyoo vya kutiririsha majitaka ambavyo vitaharibu utaratibu.

“Tayari tushafanyiwa tathmini na kila mmoja atapewa hela yake kulingana na ubora wa eneo lake huku wanaokaa upande wa chini, kushoto na kulia mwa bwawa wakitakiwa kuondoka baada ya fidia hizo na kupelekwa kwenye viwanja wanavyopewa,”  amesema Mwinyimvua.

Ofisa Ardhi Manispaa ya Morogoro, Valency Huruma, amewataka wananchi ambao bado hawajathaminiwa, watafanyiwa utaratibu huo na baadae kupewa fidia zao huku wengine waliopo ndani ya mita 500 kwenye Bwawa la Mindu wakitakiwa kuondoka baada ya kupewa fidia na kuoneshwa viwanja.

Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Morogoro, Frank Mizikuntwe,  amesema kwa sheria ya uthamini na usajili wa wathamini ya mwaka 2016 kifungu 52-53 inaelekeza baada ya ripoti kupelekwa kwa mthamini wa serikali akiidhinisha ndani ya miezi sita mthaminiwa anapaswa kulipwa na taarifa yao imeidhinishwa mwezi wa pili mwaka huu na wao watahakikisha na kulipwa baada ya miezi sita.

Ayubu Juma, mkazi wa kata hiyo ameiomba serikali kuona haja ya kulipa fidia na kuwaonesha viwanja wananchi mapema badala ya kuendelea kukaa kwenye maeneo hayo kwa wasiwasi kutokana na mvua inayoendelea kunyesha.

Juma  amesema nyumba zao zimeanza kuharibika na wao wakishindwa kuzikarabati kutokana na kuwekewa zuio la kutotakiwa kuendeleza kitu chochote mahali walipo.

Bwawa la Mindu linatoa huduma za maji kwa karibu asilimia 80 ya wakazi wa Manispaa ya Morogoro kupitia Mamlaka ya maji safi na maji taka mkoa wa Morogoro (MORUWASA).