Wanawake wapata msaada wa vyerehani, mashine za kutotolea vifaranga

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 03:43 PM Apr 29 2024


Balozi Chen na Dk. Dorothy Gwajima wakibadilisha hati kwa ajili ya kukabidhiana vifaa hivyo.
Picha: Sabato Kasika
Balozi Chen na Dk. Dorothy Gwajima wakibadilisha hati kwa ajili ya kukabidhiana vifaa hivyo.

WANAWAKE wajasiriliamali wamepatiwa vyerehani 425 na vifaa 250 vya kutotolea vifaranga, kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi.

Vifaa hivyo vimetolewa na serikali ya China na kukabidhiwa kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk.Dorothy Gwajima 

Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika leo asubuhi, katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Kijitonyama Dar es Salaam.
 
Balozi Chen nchini Chen Meijiang ndiye  aliyekavidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh. milioni 79.

Amesema, China ni rafiki wa Tanzania kwa miaka mingi, na kwamba  imekuwa ikitoa msaada wa vitu mbalimbali na kuongeza kuwa ilishatoa  mbegu za mazao ili kuongeza uzalishaji wa wa chakula nchini.

"Tumeshuhudia jinsi Tanzania chini ya  Rais Samia akijitahidi kumwezesha  mwanamke kwa kila nyanja, nasi tunaunga mkono juhudi hizo," amesema Chen.

Amesema, nchi yake itazidi kushirikiana na Tanzania kadri inavyowezekana hasa Kwa kuzingatia kwamba   urafiki wa nchi hizo mbili ni wa kihistoria na imeendelea kudumu kwa miaka mingi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima, amesema msaada huo ni sehemu ya uhusiano mzuri kwa miaka mingi.

Amefafanua kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa ahadi ya kuinua wanawake kiuchumi, na kwamba msaada huo ni mojawapo ya ahadi zake kwa wanawake.

"Mashine za kutotolea vifaranga zitagawiwa kwa vikundi ambavyo vinaratibiwa na wizara yangu, lakini vyereheni 125 vitapelekwa katika vikundi vilivyo chini ya UWT vingine 300 tutabaki navyo kwa ajili ya vikundi chini ya wizara yangu," amesema.

Mwenyekiti wa UWT, Mary Chatanda, amesema kuwezesha wanawake ni sawa na kuongeza kasi ya kupata asilimia 50 kwa 50 katika uongozi.

"Wanawake wanakwama kufikia lengo hilo kwa sababu za kiuchumi, suala hili linahitaji fedha, kwa njia hii ninaami I tunaelekea kuipata hiyo asilimia," amesema Mary.