Watatu wafariki dunia kwa kuangukiwa na ukuta

By Halima Ikunji , Nipashe
Published at 12:44 PM May 02 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao
PICHA: MAKTABA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao

WATU watatu wamefariki dunia kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba katika Kijiji cha Iyombo Nyasa Kata ya Utwigu wilayani Nzega.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema watu hao walifikwa na umauti nyakati za usiku wakiwa wamelala, aliwataja waliofariki ni Rashidi Matoma, Chiku Mihayo na Hamisi Rashidi.

Abwao amesema tukio hilo lilitokea wakiwa wamelala na chanzo cha ajali hiyo ni mvua kubwa kunyesha na kusababisha ukuta kuwaangukia.

Amesema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na uchunguzi wa daktari ulibaini sababu ya vifo hivyo ni majeraha makubwa kichwani baada ya kudondokewa na ukuta na damu kuvuria katika ubongo.

Hivyo, ametoa wito kwa wanafamilia wanapopata matatizo wahakikishe wanakwenda kwa viongozi wa dini au wakiserikali kwa ajili ya kupata ushauri na siyo kujichukulia sheria mkononi.

Aidha, mewaasa wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua na kuhakikisha watoto wao wanakuwa salama na wasicheze sehemu yenye mashimo ya madimbwi.

 Pia  amesema katika mkoa wake hali ya usalama inaendelea vizuri japokuwa matukio machache yanaendelea kujitokeza.