Waziri wa Fedha wa zamani Mkulo afariki dunia Dar

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 08:44 AM May 05 2024
WAZIRI wa Fedha wa zamani, Mustafa Mkulo.
PICHA: MAKTABA
WAZIRI wa Fedha wa zamani, Mustafa Mkulo.

WAZIRI wa Fedha wa zamani, Mustafa Mkulo, amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akiendelea na matibabu ya maradhi yaliyokuwa yakimkabili.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa mke wake, Julie Mkulo, mume wake alifariki dunia juzi hospitalini hapo na shughuli za mazishi zilifanyika siku hiyo Dar es Salaam na anatarajia kuzikwa leo Kilosa mkoani Morogoro.

“Shughuli zote za mazishi zitakuwa msikiti wa Maamur leo (jana) na maziko yatafanyika kesho (leo) Kilosa,” amesema.

Mkulo alikuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Nne na ni mbunge mstaafu wa Kilosa (CCM) aliyetumikia wana Kilosa kwa kipindi cha miaka 10 tangu mwaka 2005 na kutangaza kustaafu wadhifa huo mwaka 2015.

Moja ya sababu ya kustaafu ubunge aliwahi kutaja ni kwa kuwa wakati huo idadi kubwa bungeni ni ya vijana, hivyo kwa umri wake aliona kuwaachia kuchukua nafasi hiyo.

Ni mwenye Shahada ya Uzamili kwenye masuala ya fedha aliyoipata katika Chuo Kikuu cha SouthWest, London, Uingereza kati ya mwaka 1975 na 1977.

Alishika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo kuwa Naibu Waziri wa Fedha 2006- 2008 na kuteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na baadaye alienguliwa kutokana na tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikimkabili.

Aidha, kwa muda mrefu Mkulo alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa uliokuwa Mfuko wa Taifa wa Pensheni kwa Wafanyakazi (NPF) kabla ya kuwa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) hadi alipostaafu mwishoni mwa miaka ya 1990 .