Zitto kujitosa urais uchaguzi mkuu 2025

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 11:35 AM May 06 2024
MWENYEKITI mstaafu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
PICHA: MWANDISHI WETU
MWENYEKITI mstaafu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

MWENYEKITI mstaafu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema yupo tayari kuipeperusha bendera ya chama hicho katika nafasi ya urais wakati wa Uchaguzi Mkuu mwakani, endapo wanachama watampa ridhaa hiyo.

Ametoa kauli hiyo na wakati wa sherehe za kutimiza miaka 10 ya chama hicho zilizofanyika mkoani Kigoma na kuhudhuriwa na wanachama, viongozi mbalimbali wa chama hicho kutoka Bara na Visiwani.

Zitto amekuwa akisikika akitangaza nia ya kuwania ubunge katika Jimbo la Kigoma Mjini alilowahi kuliongoza mwaka 2015 hadi 2020, lakini jana ilikuwa tofauti akisikika kutangaza kuwania urais.

Amesema licha ya kustaafu kwake kwenye uongozi hatosita kufanya jambo lolote litakalokuwa na maslahi ya chama na nchi endapo viongozi wataona anafaa kutumika katika jambo hilo.

“Nimejiandaa kisaikolojia, kiakili na kimaarifa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wowote viongozi wangu mkinihitaji nipo tayari kuwahudumia,” amesema Zitto.

Kuhusu uamuzi wake wa kuingia katika kinyang'anyiro hicho, Zitto amesema utatokana na matakwa ya wananchi na kutimiza malengo ambayo chama hicho kimejiwekea kwa miaka 10 ijayo ikiwamo kushika dola na kuiletea nchi maendeleo.

Amesema wakati chama hicho kinaanzishwa watu walikiita ni chama cha wana Kigoma, lakini sasa kimekuwa na viongozi na wawakilishi nchi nzima, akisema ni jambo la kujivunia.

"Kiongozi wa chama ni mtu kutoka Kilimanjaro, Mwenyekiti ni mtu kutoka Pemba, Makamu Mwenyekiti Bara ni mtu kutoka Lindi, Makamu Zanzibar ni mtu kutoka Unguja, Katibu Mkuu katoka Tunduru. Wanachama mjivunie mbegu mliyoipanda kwa miaka 10 iliyopita kwa sasa imeenea Tanzania nzima mnapaswa kutembea kifua mbele," amesema Zitto.

Naye Mwenyekiti wa chama hicho, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Massoud Othman, amesema msimamo wa chama hicho ni kuhakikisha kuwa kunapatikana Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi ili Watanzania wanakuwa na uhuru wa kumchagua rais wamtakaye.

Amesema ili hilo liwezekane chama hicho kinapaswa kuwa madarakani katika uchaguzi ujao na kuwasihi wanachama wa chama hicho kuhakikisha wanachagua viongozi wa chama hicho kwa kishindo katika uchaguzi ujao.

"Mungu akipenda mwaka 2025 tunataka tushindane na Kigoma, mkikabidhiwa serikali kule (Zanzibar) huku Kigoma pia (Bara) mtukabidhi kwa sababu ng'ombe hachinjwi mkiani," amesema.

JUSSA AAHIDI USHINDI

Makamu Mwenyekiti wa ACT Zanzibar, Ismail Jussa, amesema kwa upande wa Zanzibar wamejipanga kuhakikisha kuwa katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwakani chama hicho kitachukua madaraka chini ya Mwenyekiti wao, Othman Masoud Othman ili kuwaletea wananchi maisha wanayostahili.

Aidha, amewataka wananchi wa Kigoma kuhakikisha kuwa wanampitisha Mwenyekiti mstaafu, Zitto Kabwe kuwa mbunge wa jimbo hilo pamoja na kumpitisha kwa kishindo katika nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu mwakani.