Daktari bingwa achambua wasiyojua watu wengi ndani ya ugonjwa kifafa

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 09:25 AM May 09 2024
news
Picha: Christina Mwakangale
Tabibu bingwa wa maradhi ya ubongo, Dk. Patience Njenje.

WANAOUGUA kifafa wanaelezwa wana hatari ya vifo, mara sita zaidi ya wengine. Tabibu bingwa wa maradhi ya ubongo, Dk. Patience Njenje, anabainisha katika mazungumzo na Nipashe, akitaja mahususi maradhi yako katika kiwango cha asilimia 60.

“Kuwa na kifafa ni hatari. Kifo ni muda wowote…ikilinganishwa na ambao hawaugui ugonjwa huo,” anasema bingwa.

Anaendelea kwa ufafanuzi: “Utakuta mtu alikuwa amepanda juu ya mti, akaanguka ghafla, au anaendesha gari, lakini ana kifafa, kinamkamata wakati anaendesha gari, mwendokasi mkubwa, anapata ajali.”

Dk. Njenje anasema, ugonjwa huo humkumba anayeugua muda wowote, akitumia mfano wamo waliokuwa wanaogelea, wakadhurika na maji, wakazama na hatimaye kifo.

Kwa mujibu wa daktari huyo, asilimia mkubwa ya wanaougua anawataja ni vijana kuanzia umri wa miaka 15, akibainisha, baadhi yao huangukia kwenye moto na kukosa msaada wa kuwanusuru.

“Mwenye kifafa anaanguka! Akianguka anapoteza fahamu. Anakuwa hajijui. Akiangukia kwenye moto ataungua, akiungua atapata madhara, makovu au ulemavu!

“Asilimia zaidi ya 25 wanaougua kifafa wana ulemavu. Ukiwachukua wote wanaougua milioni 60 duniani, kati yao asilimia 25 wana ulemavu,” anafafanua bingwa huyo ambaye anahudumia kliniki ya PCMC, iliyoko Upanga, jijini Dar es Salaam.

“Watu wanaoishi na kifafa ni zaidi ya watu milioni 60 duniani kote na ni ongezeko la watu 34 hadi 76 kwa kila watu 200,000 kwa mwaka. Kaulimbiu ya mwaka – 2024 ni ‘Tulikotoka, tulipo na tunakoelekea.”

Anasema, uhalisia huo mwilini anakuwa nao mgonjwa, hata kumjengea vikwazo kimaisha, kwamba: “Huu ni ugonjwa wa kibaolojia. Hizo ni dhana tu. Kwenye ubongo huwa kuna shida, labda kuna uvimbe, hitilafu ya mfumo wa umeme.

“Ikitokea basi mtu atapata shida. Uchawi, mapepo ni imani potofu, ni dhana tu. Asilimia 50 katika jamii watu wanamini kifafa ni ugonjwa wa kuambukiza.

“Kifafa ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza. Mimi mwenyewe nikiwa shule ya bweni nilikuwa nakimbia, niliamini mtu mwenye kifafa akianguka utaambukizwa, tuliamini akijisaidia, akitoa hewa chafu utaambukizwa,” anasema.

“Lakini kwa sababu nilienda shule, sasa ninajua, nimeelimika. Kifafa kikikukamata, maana yake, misuli yote inakakamaa, ndio maana mtu anajisaidia, kama tumbo lilijaa ataishia kujisaidia haja ndogo au kubwa.”

Anasema, wanaougua pia hunyanyapaliwa, wakikosa tofauti kama vile elimu na wanatengwa na jamii hata familia zao.

“Mtu anatakiwa aripoti shule fulani, anaambiwa ‘hapana, nenda shule nyingine.’ Utakuta mwalimu mkuu (au mkuu wa shule) anakataa, anaonekana ataambukiza watu. 

“Kuna unyanyapaa, wengine wanafukuzwa kazi. Lakini ni ugonjwa kama magonjwa mengine, kama kifafa hakiambukizi…kama ni hivyo basi wenye presha, kisukari, saratani wafukuzwe.

“Afrika ni mojawapo, ina asilimia kubwa ya watu wanaoishi na kifafa. Inafahamika ni watu 20-58 kwa kila watu 1,000,’ anasema na kuendelea:

“Pia, Tanzania ina idadi kubwa ya wagonjwa wa kifafa katika Afrika na dunia, mojawapo kati ya nchi zenye wagonjwa wengi zaidi.”

Bingwa huyo anatumia mifano, kwamba, kwenye vijiji vya Wilaya ya Mahenge, mkoani Morogoro, vina idadi kubwa ya wenye vifaa, wastani wa watu hadi 37, katika kundo la kila watu 1,000, hali inayotajwa kuwafanya watu zaidi ya milioni moja Tanzania, wanaugua.

Kuhusu matibabu, bingwa huyo anasema asilimia tano pekee ndio wanaofika hospitalini, wengi kwenye tiba za kiimani tofauti, kama vile kuombewa makanisani na misikitini, au kwenye tiba za kienyeji.

Mtazamo wake daktari kitalamu ni kwamba, maradhi kifafa kisipewe uhusiano na homa za watoto, ambazo mara nyingi huwasababishia degedege.

Anataja aina ya uhusiano ulioko ni kwamba, panapokuwapo homa kali kwa mtoto, hata kumsababisha apoteze fahamu, ni hatari inayoweza kumsababishia kuwa na kovu kwenye mishipa ya ubongo hatimaye, kifafa.

HALI ZAO ZILIVYO

Bingwa huyo anaeleza, watoto wenye umri wa kwenda shule wenye tatizo hilo, kwa asilimia 45 hawapelekwi shule. Vilevile, asilimia 68 ya mahudhurio yao hayaridhishi, huku asilimia 37 ndio hupata elimu za msingi.

“Watoto hawa hawaruhusiwi kucheza na wengine, hivyo hufichwa katika jamii. Asilimia 75 ya wagonjwa huenda kuwaona waganga wa jadi na wengine huenda kuwaona viongozi wa kiroho (dini).

“Kuna watu wengi ambao wana shida ya kifafa kidogo. Sio hadi aanguke, wengine wanapoteza fahamu, wengine wanatikisika tu, labda mkono. Inapotokea kaanguka. usimshikilie, usimzuie, ana hatari ya kufyatuka bega wakati huo. 

“Muache ajing’ate, atapona. Usimshikile, mlaze ubavu wa kushoto, asilale chali. Akizinduka mpeleke hospitali,” daktari huyo anatafsiri uhalisia na hali ya awali, akiendeleza ufafanuzi kuwa: 

“Tunawafundisha pia wagonjwa wa kifafa kwamba, kwanza usiendeshe gari hatujui lini kitakushika, usiogelee, usipande magorofani au majengo marefu, ngazi, asikwee.”

Anatoa angalizo kwamba, si kila anayeanguka au kupoteza fahamu, mgonjwa wa kifafa, huku akitoa mbinu za kujikinga na visababishi vinavyozuilika ni kama vile, kumjali mama mjamzito kipindi chote cha ujauzito na kuhudhuria kliniki.

 “Ugunduzi na matibabu ya haraka kwa watoto wanapopata homa, kuhimiza choo bora na kwa wale wanaokula nyama ya nguruwe iive, kuacha kuwabagua wagonjwa. Serikali ihakikishe uwapo wa utoaji dawa za kutosha kutibu wagonjwa hawa,” anasema.