MWANASIASA MWAMI TEREZA NTARE Kielelezo cha hitaji la kuandika upya historia ya wanawake Tanzania

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:56 AM Apr 24 2024
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, katika maadhimisho ya mafanikio ya Mwami Tereza, pamoja na wadau mbalimbali kuenzi michango  yake na ya wanawake walioshiriki katika harakati za ukombozi wa Tanganyika.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, katika maadhimisho ya mafanikio ya Mwami Tereza, pamoja na wadau mbalimbali kuenzi michango yake na ya wanawake walioshiriki katika harakati za ukombozi wa Tanganyika.

MWAKA 1958 uchaguzi unafanyika ili kumpata kiongozi mkuu wa machifu wote wa Tanganyika. Zilikuwa zama za ukoloni wa Waingireza na mwanamama Mwami Tereza Ntare II, Chifu wa Jamii ya Heru wa Kigoma anaibuka kidedea. Akiwaangusha machifu wanaume.

Wakati huo Tereza  alikuwa chifu pekee mwanamke na kwa kura nyingi anachaguliwa kuwa  Mkuu wa Machifu wote Tanganyika, akichuana na Chifu Marealle wa Marangu mkoani Kilimanjaro.

Kuanzia zama hizo hadi sasa ni miaka 66, licha ya leo kuwapo teknolojia na hata ushiriki wa wanawake katika siasa kuongezeka tofauti na wakati wa ukoloni, cha kushangaza idadi ya kinamama inazidi kuporomoka kwenye uwanja wa siasa na mara nyingi wakigombea uchaguzi majimboni wanashindwa.

Ni tafakuri inayoibuka kwenye jukwaa la kusherehekea mafanikio ya Mwami Tereza Ntare linaloandaliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Makumbusho ya Taifa na familia ya Tereza, jijini Dar es Salaam hivi karibuni. 

Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo akiwa Waziri  wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, anawatafakarisha washiriki wa maadhimisho hayo akihoji:

“Ikiwa mwaka 1958 mwanamama Mwami Tereza alishinda uchaguzi  kwa kura nyingi kwa asilimia 89 na kuwa kiongozi wa machifu, nini kilifanyika wakati huo? Leo kikwazo nini idadi ya wanawake kwenye uchaguzi haijaongezeka? 

Anasema kuna mengi ya kujifunza, mojawapo ni ujasiri, uthubutu , upambanaji na kujiamini.Anawaambia washiriki kuwa wanawake wanaweza kupata ukombozi kwa kufanya mambo hayo na pia kuungwa mkono na jamii kama Tereza alivyoungwa mkono na jamii ya machifu wa Tanganyika wakati huo.

Anamwita Mwami Tereza shujaa ambaye licha ya kusoma Ulaya alicha masomo na kurudi ili kuongoza jamii na taifa lake, baada ya kifo cha baba yake mwaka 1947, akiwa ni mzalendo aliyejali maslahi ya wengi na siyo yake.

Anasema licha ya kwamba historia yake haifahamiki ni mwanamke wa kwanza kujiunga na chama cha TANU na kuieneza kwa watu wa Ukanda wa Magharibi ya Tanganyika.

Aidha, alishirikiana na machifu wengine kueneza ujumbe wa TANU wa kuleta uhuru wa Tanganyika .

Waziri Ndumbaro anasema kazi za mwami Tereza ni alama ya kishujaa inayoonyesha kuwa wapo wanawake wana mapinduzi, wapigania uhuru waliojitoa kuleta uhuru wa Tanganyika na Afrika ili kuwaondoa watu kwenye ukoloni.

KUANDIKA HISTORIA

Akizungumzia kazi za Mwami Tereza kukosekana kwenye historia ya Tanzania, Dk. Ndumbaro anasema:

“Ni kutokana na sisi kutoandika kazi zetu, tuondoe uvivu hata sasa tunawaachia wengine waandike historia yetu kwenye mitandao.”

Nitoe mfano” “Kulikuwa na ziara ya kiongozi mashuhuri kutoka Marekani aliyekuja Tanzania na taarifa kwenye mitandao zikaripoti kuwa kiongozi huyo anatembelea kijiji cha wavuvi cha Dar es salaam. ….is visiting the largest fishing village of Dar es salaam”

Anasema huo ni upotoshaji, unaotokea kwa sababu watu hawaandiki wenyewe historia matukio , harakati na masuala yote yanayolihusu taifa. 

Ili kuondoa upotoshaji na hata kutoandikwa kwa kazi za kishujaa kama ilivyotokea kwa Mwami Tereza watu waanze kuandika sasa.

Akireja uchache wa wanawake kwenye uwanja wa siasa,  Mkurugenzi wa Shirika la Women Fund, Rose Marandu, anasema wanawake waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa 2020 ni  26 pekee kati ya 264 waliopigiwa kura majimboni. 

Akitazama uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, ukifuatiwa na uchaguzi mkuu mwakani, Rose anatoa angalizo.

Anasema chaguzi hizo zinajiri wakati wanawake kwenye sekta ya uongozi wa serikali za mitaa ni ndogo mno, ni asilimia mbili pekee ya wenye viti wa vijiji  na asilimia 6.7 ya wenye viti wa vitongoji.

Kwa mujibu  Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Tanzania ina vijijini 12,319,  vitongoji viko 64,384 wakati mitaa ni  4,263. 

Kwa idadi hiyo ya vijiji, wanawake wenyeviti ni wachache mno ni takribani 246 pekee kwa Tanzania nzima, Rose akitafsiri hali hiyo kuwa kukosa uwiano na kuzidi kukwamisha jitihada za kufikia usawa kwa uwakilishi wa 50/50 baina ya wanawake na wanaume kwenye uongozi na uwakilishi.

Anaishauri serikali kuona umuhimu wa kutoa hamasa na elimu kwa wanawake ili waweze kufikia ndoto zao , kuweka mazingira na miundombinu wezeshi  ili kuwafikisha kwenye ushiriki wa masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ili kupata viongozi kama Mwami Tereza.

MAMBO MAKUBWA

Katika maadhimisho ya mafanikio ya Mwami Tereza, mambo mengi aliyoyafanya yalibainishwa kwa mfano, alinunua kadi 3,000 za TANU na kuzisambaza kwa wananchi usiku wa manane, huko Kigoma ili washiriki uchaguzi mkuu wa 1958.

Taarifa zake zilimfikia Mkuu wa Wilaya ya Kasulu DC mkoloni wa Kiingereza aliyevamia nyumba yake na kutaka kuipekua.

Mwami alidaiwa kukuwsanya kadi na kuzilalia akihoji inakuwaje apekuliwe usiku, hata hivyo DC na jeshi lake walikimbia baada ya wananchi kujipanga na silaha za jadi kukimbilia nyumbani kwa Tereza kumnusuru baada ya kusikia kuwa amevamiwa usiku wa manane.

Kutoa kadi hizo kuliwezesha watu kuzitumia kupiga kura mwaka 1958 na kukipa chama cha TANU ushindi mkubwa.

Mwami Tereza anatajwa kuwa msomi wa sheria aliyejua haki za binadamu na kuzitetea alitumia elimu yake kueneza TANU mikoa ya Tabora, Shinyanga na Rukwa pia alishiriki katika misafara ya kuomba kura, kuhimiza watu kuiunga mkono TANU na kuwashawishi machifu wengine kushiriki kwenye harakati za kupigania uhuru.

Aidha, anatajwa kuwa mwanamke shujaa na alama ya ukombozi wa Tanganyika, ambaye baada ya chama cha TANU kuanzishwa 1954, alikuwa mwanamke wa kwanza kujiunga akiwa mstari wa mbele kuieneza kwa machifu wengine.

Kiongozi huyo ambaye licha ya machifu kukatazwa kujihusisha na siasa kwa sheria iliyotungwa na wakoloni  alisimamia ustawi wa TANU na kuiimarisha.