Maofisa mikopo wapigwa msasa kukopesha wakulima

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:49 PM May 06 2024
Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kaanaeli Nnko, akihutubia maofisa mikopo 52 kutoka benki washirika 20, ambao walishiriki katika mafunzo yaliyolenga kuwaongezea uelewa juu ya utoaji wa mikopo ya kilimo kwa wakulima nchini.
PICHA MAULID MMBAGA
Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kaanaeli Nnko, akihutubia maofisa mikopo 52 kutoka benki washirika 20, ambao walishiriki katika mafunzo yaliyolenga kuwaongezea uelewa juu ya utoaji wa mikopo ya kilimo kwa wakulima nchini.

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ikishirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wamewapatia mafunzo maofisa mikopo 52 kutoka benki washirika 20 kwa lengo la kuwaongezea uelewa wa kutoa mikopo ya kilimo kwa wakulima nchini.

Vilevile, mafunzo hayo yanalenga pia kuzijengea uwezo taasisi za fedha ili kuziongezea maarifa na ujuzi kwa wataalamu wa fedha kwenye kilimo ili kuchagiza ongezeko la upatikanaji huduma za fedha, mikopo na rasilimali watu kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi nchini.

Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa TADB, Kaanaeli Nnko, alisema lengo la programu hiyo ni kuhakikisha wakulima wanafikiwa katika mikoa yote.

Nnko, alisema hadi sasa mfuko wao umedhamini mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 270 kupitia kwa benki washirika.

Alisema mikopo ya kilimo ni tofauti na ya kawaida, hivyo moja ya maeneo yaliyozingatiwa katika mafunzo hayo ni kuangalia namna gani ya kupunguza hatari ambayo itawawezesha watoa mikopo kubaini viashiria hatarishi na kuweza kuvizuia ili taasisi zisipate hasara.

"Hadi tunapozungumza tumeweza kufikia wakulima walengwa 24,000. Na tunaamini kwa haya mafunzo na washiriki tutakuwa na mafanikio zaidi, kwenye sekta ya kilimo hadi sasa benki washirika wametoa asilimia 11 ya mikopo na lengo letu ifikapo 2030 sekta ya mikopo yote inayotolewa itakuwa imefika asilimia 30," alisema Nnko.

Makamu Mkuu wa Chuo cha BoT, Dk. Ephraim Mwasanguti, alisema TADB iliwapatia jukumu la kutengeneza programu kwa ajili ya wakulima wadogo ikilenga kuwaelimisha maofisa mikopo wa benki washirika wanaosimamia skimu ya mikopo ya TADB ili watoe mikopo ambayo italipika.

Meneja Uhusiano Kilomo Biashara Benki ya CRDB, Salvatore Silvester, ambaye ni miongoni mwa walioshiriki mafunzo hayo, alisema programu hiyo imewasaidia kufungua mtazamo wao kukiangalia kilimo tofauti.

Mafunzo hayo kwa awamu ya kwanza yametolewa na wakufunzi kutoka BoT Academy, wataalamu kutoka Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA) na Chuo cha Mtakatifu Agustino (SAUT) kuanzia Aprili 22 hadi Mei 3, mwaka huu.