Azam yapania makubwa msimu ujao michuano CAF

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 06:45 AM May 04 2024
news
Picha: Mtandao
Wachezji wa Azam FC.

HAWATAKI utani, ndio kinachoonekana ndani ya Azam FC ambayo imejipanga kujiimarisha kwa kufanya usajili 'mkubwa' kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa watakayoshiriki.

Baada ya kuhusishwa kuweka mezani ofa kuhitaji huduma ya wachezaji wawili wa Simba, Aishi Manula na Kibu Denis, Azam inatajwa imeanza kuwinda sahihi ya beki wa Yanga, Kibwana Shomari.

Taarifa zilizopatikana jijini, Dar es Salaam zinasema Azam imeanza mchakato wa kumsajili Kibwana na mazungumzo yamefikia katika hatua nzuri.

Chanzo hicho kilisema Azam inaamini ikimpata beki huyo wa pembeni itafanikiwa kuongeza nguvu kikosi chake ili kifikie malengo.

"Uongozi unafuatilia kwa karibu suala la Kibwana, inafahamika bado hajasaini mkataba mpya na Yanga, na kama watachelewa inawezekana msimu ujao akachezea Azam.

Tunataka Azam FC ya msimu ujao iwe ya tofauti sana na ndio maana mipango imeanza mapema kukisuka kikosi chetu, lakini pia kuna uwezekano mkubwa wa kushiriki mashindano ya kimataifa, tunataka kufanya vizuri kwa sababu mara nyingi tumekuwa tukiishia hatua za awali," kilisema chanzo chetu kutoka kwa klabu hiyo ya Chamazi.

Hata hivyo kuhusu usajili wa Kibwana na nyota wengine, Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, alisema uongozi wa timu hiyo unaendelea na mazungumzo kuhakikisha inawabakisha wachezaji wote inaowahitaji na ambao mikataba yao inaelekea ukingoni.

"Niwatoe hofu mashabiki na wanachama wa Yanga, uongozi wetu upo makini sana, hakuna mchezaji tunayemhitaji ataondoka Yanga, wale wote ambao tunaona wanahitajika ndani ya klabu watabaki na tutakuwa nao msimu ujao," alisema Kamwe.