Aziz Ki 'hatari' mabao mashuti ya mbali Bara

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:09 AM May 04 2024
Aziz Ki.
Picha: Maktaba
Aziz Ki.

KINARA wa mabao wa Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa, Stephane Aziz Ki, anaongoza kwa kufunga mabao kwa mashuti ya mbali katika ligi hiyo inayoelekea ukingoni.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Bodi ya Ligi Kuu jana, pamoja na za dawati la michezo la Nipashe, zinaonyesha raia huyo wa Burkina Faso huyo amefunga mabao matano akiwa nje ya boksi mpaka sasa. 

Aziz Ki, ambaye amepachika mabao 15 mpaka sasa katika ligi hiyo, ni mmoja wa wachezaji ambao ni hatari kwa kupiga mashuti ya mbali, akiwa anakokota mpira, au kwenye mikwaju ya faulo.

Wakati Aziz Ki, aliongoza kwa mabao ya mashuti ya mbali, kiungo mshambuliaji mwingine wa Ihefu FC, raia wa Togo, Marouf Tchakei, anafuatia akiwa na mabao matatu ambayo ameyapachika akiwa nje ya boksi.

Wachezaji watano wanakamata nafasi ya tatu kwa kukwamisha wavuni mabao kwa mashuti ya mbali, nao ni Edwin Barua wa Simba, moja akilifunga akiwa kwenye timu yake hiyo mpya na lingine alipotoka, Prisons, pamoja na Clatous Chama, wote wakitokea Wekundu Msimbazi, wakiwa wamepachika mabao mawili, kila mmoja.

Wengine waliopachika mabao mawili, ni Valentino Mashaka na Tariq Seif, wote wa Geita Gold, Kipre Junior na Azam FC.