Gunners bingwa Ligi ya Mikoa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:58 AM Apr 19 2024
Timu ya Gunners, ambao  wametwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Mikoa.
Picha: TFF
Timu ya Gunners, ambao wametwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Mikoa.

WENYEJI Gunners wametwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Mikoa baada ya kuifunga Hausung FC ya Njombe bao 1-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma juzi.

Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa na Fadhili Suleiman dakika ya 25, hata hivyo timu hizo mbili zilizocheza fainali zimepanda daraja na zitashiriki Ligi Daraja la Pili 'First League' msimu ujao.

Timu nyingine iliyofanikiwa kupanda daraja ni Moro Kids ambayo iliiadhibu Arusha City mabao 3-0 katika mechi ya awali kutafuta mshindi wa tatu.

Mabao ya washindi yalifungwa na Said Hamisi, aliyepachika mabao mawili dakika ya 38 na 90, na Mohamed Salehe aliyefunga goli dakika ya 59.

Mchezaji wa Gunners, Costa Mwihoneke, alipata tuzo mbili kwa kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo, pamoja na mchezaji bora huku tuzo ya kipa bora ilikwenda kwa Mudhihir Jaffar wa Gunners na kocha wa timu hiyo, Juma Ikaba ambaye ni kiungo wa zamani wa CDA ya Dodoma, alichaguliwa kuwa kocha bora.