Serikali yaanika mkakati Stars kuwika Afcon 2027

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 06:59 PM Apr 30 2024
Timu ya Taifa (Taifa Stars).
Picha: Maktaba
Timu ya Taifa (Taifa Stars).

MBUNGE wa Magomeni (CCM), Mwanakhamis Kassim Said, amehoji mikakati ya serikali ya kuihamasisha Timu ya Taifa (Taifa Stars), ili ifanye vizuri katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, kama inavyofanyika kwa Klabu za Simba na Yanga kwenye michuano ya kimataifa.

Akiuliza maswali bungeni jana, mbunge huyo alisema ili mashindano hayo yafane nchini, lazima kuwe kuna timu inayoshiriki na kuhoji mkakati wa serikali wa kuisimamia timu ya taifa.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA, alisema Tanzania kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda zitakuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027.

“Ili kuhakikisha timu ya taifa inafanya vizuri katika mashindano hayo, serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwamo; ujenzi wa viwanja vya mpira katika majiji ya Dodoma na Arusha, ukarabati wa viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru pamoja na kuwatafuta na kuwaleta nchini wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaoishi na kucheza nje ya nchi ili kuichezea timu ya taifa.

“Kuhakikisha timu ya taifa inashiriki mechi za kirafiki na mataifa mbalimbali na kufanya kambi katika mazingira mazuri ili kuwa na maandalizi bora,” alisema Mwana FA.

Alitaja mkakati mwingine kuwa ni kuwashirikisha wadau mbalimbali wa michezo kuchangia timu za taifa kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha za kuzigharamia timu za taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa.

Pia alisema kuwa uwenyeji wa mashindano ya CHAN mwaka 2024 ambayo ni maandalizi kwa timu ya taifa kuelekea AFCON 2027, kuajiri kocha na benchi la ufundi lenye sifa na uzoefu katika mpira wa miguu duniani na kuhudumia timu zote za taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa.