Vita Ligi Kuu Wanawake kuendelea viwanja vitano

By Saada Akida , Nipashe
Published at 06:26 AM Apr 19 2024
Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi'.
Picha: Simba SC
Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi'.

RAUNDI ya 11 ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara itaendelea tena leo ambapo mabingwa watetezi, JKT Queens watakuwa nyumbani kuwakaribisha Geita Gold FC huku Simba Queens ikiwavaa wenyeji Baobab Queens kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma jijini, Dodoma.

Amani Queens watawakaribisha Yanga Princess katika dimba la Ilulu mkoani, Lindi huku Ceasiaa Queens ya Iringa bado wako nyumbani kucheza dhidi ya Fountain Gate Princess na Alliance Girls watawaalika Bunda Queens kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini, Mwanza.

Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi', alisema wamewasili salama Dodoma na wachezaji wake wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo huku lengo lao kubwa ni kutafuta pointi tatu.

Mgosi alisema ajenda yao ya kwanza katika mzunguko wa pili wameianza kwa mafanikio ambapo walipata ushindi wa bao 1-0 ugenini na sasa wanahitaji kutafuta alama tatu nyingine watakapoivaa Baobab Queens.

“Tangu msimu unaanza ninasema tunahitaji kurejesha heshima ya klabu, kufikia malengo hayo lazima tushinde mechi, hatuwadharau Baobab Queens licha ya kupitia changamoto nje ya uwanja, tutacheza kwa tahadhari kubwa,” alisema Mgosi.

Kocha Mkuu wa JKT Queens, Esther Chabruma, alisema kutokana na maandalizi waliyofanya, anaimani kikosi chake kitaendelea kubakiza pointi tatu katika uwanja wao wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Chabruma alisema mechi ya kwanza walifanikiwa kuvuna pointi tatu na sasa wanahitaji ushindi kwa ajili ya mipango yao ya kuhakikisha wanatetea taji la ubingwa wanalolishikilia.

"Bado hatujakata tamaa katika mbio za ubingwa, ligi inaendelea na tumejiandaa vizuri na mchezo wetu dhidi ya Geita Gold FC, kikubwa ni kuvuna pointi tatu,” alisema Chabruma.

Kocha wa Fountain Gate Princess,  Alex Alumirah, “ Ni mechi ngumu,Ceasiaa Queens ni timu nzuri ukiangalia katika msimamo wako nafasi ya nne, sisi tupo ya tano, tunahitaji kupanda juu lazima tushinde hii mechi.

Nafurahi mechi ya kwanza hatukuruhusu bao na wala kufunga, tumefanyia kazi mapungufu yetu na sasa tuko tayari kwa mchezo huo wa ugenini,” alisema Alumirah.