Hatari ya vijana kutoshiriki kikamilifu shughuli za kisiasa

By Magabilo Masambu , Nipashe Jumapili
Published at 04:57 PM Feb 04 2024
Vijana
Mtandao
Vijana

VIJANA ndiyo taifa la kesho. Wazee na viongozi wa leo walikuwa vijana miaka iliyopita, kwa hiyo walikuwa vijana kabla ya kuwa wazee japo kuna wakati maisha yanaweza kumfanya kijana akaonekana mzee na mzee akaonekana kijana kwa mwonekano wa nje na ndani.


Mara kadhaa nimesikia baadhi ya wanasiasa wazee wakiwataka vijana kutojihusisha na siasa na kwamba siasa ni kupoteza muda. Wanaosema hayo wako kwenye siasa toka ujana wao na hawajawahi kuona kama wanapoteza muda na kujaribu kutafuta kazi zingine ambazo si za kupoteza muda. Jambo hili linanipa wasiwasi juu ya wazee wajao, watakuwa wazee na viongozi wa namna gani katika siasa, ikiwa vijana wanaambiwa siasa ni kupoteza muda.

Tutakubaliana kwamba siasa ni maisha na maisha ni siasa. Hakuna jambo linafanyika kwenye dunia hii bila kuhusika na siasa. Uwe  unafanya biashara, kilimo, ufugaji, msomi na kadhalika lazima siasa inahusika kwa sababu uamuzi wa ambo yote unategemea viongozi wa kisiasa. Kwa hiyo jaribio lolote la kuwataka vijana kutojihusisha na siasa ni kujaribu kuyakataa maisha yao wenyewe.

Kuna wakati walioko madarakani wanaweza kuona ni jambo zuri na la afya kuwa na vijana makondoo wasiojua kuhoji, wasiouliza chochote kuhusu siasa au maisha yao lakini athari zake kwa taifa huko mbeleni ni kubwa. Katika nyakati hizi za mfumo wa vyama vingi, vijana wanaokuwa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za siasa kwenye vyama vyao, watakuwa na ujasiri wa kulitetea taifa wanapopata nafasi ya madaraka serikalini. Kwa mantiki hiyo, ni muhimu kushirikishwa na wao kushiriki vyema katika masuala ya kisisasa.

Vijana kutoshiriki katika shughuli za siasa, si hasara tu kwa vyama vya upinzani bali hata chama tawala. Madhara yameshaanza kuonekana pale vyama vinapofanya mikutano. Vijana  wengi hawajitokezi na hiyo si ishala nzuri. Taasisi  za elimu kama vyuo vikuu ambazo zilikuwa kama jiko la kupika viongozi, leo hii vijana katika taasisi hizo hawashiriki kikamilifu katika makongamano mbalimbali kama ilivyokuwa zamani. Hapo lazima tuone kuna tatizo na pengine litafutiwe dawa.

Utaratibu wa kutumia vitisho kwa vijana wenye mawazo mbadala au yasiyokubaliana na utawala katika taasisi mbalimbali za elimu kutoka shule za msingi mpaka vyuo vikuu, haujengi vijana shupavu kwenye taifa badala yake unajenga vijana waoga wasiokuwa wabunifu kwa sababu tayari wanakuwa na uoga wa kuanzisha jambo lolote. Kwa kujengwa hofu, vijana wanakuwa na mawazo tegemezi. Kila  wanachofikiria kufanya wanahisi watakosea na wanahitaji maelekezo kutoka kwa mtu fulani.

Baada ya kipindi fulani cha siasa za nchi yetu, sasa naona tumeanza vizuri pengine mwelekeo huu utaturudisha katika siasa za wakati wa awamu ya nne ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati ambao tuliona uhusika wa vijana wengi katika siasa za Tanzania. Ndio  wakati ambao bunge lilikuwa na mvuto kwa Watanzania, wananchi waliacha shughuli zao nyakati za vipindi vya bunge na kuwenda kufuatilia. Ni wakati ambao Watanzania wengi walikuwa wanajitokeza kwenye mikutano ya vyama vya siasa. Siasa za upinzani zilipamba moto na ni kiu yangu nione kipindi kama hicho tena maana ni afya kwa taifa kwa kuwa wananchi wataanza kufuatilia mambo ya msingi yanayoathiri maisha yao ya kila siku.

Nazikumbuka siasa za Arusha, Mbeya, Mwanza, Dar es Salaam pamoja na kuwa na mwitikio mkubwa wa majukwaani kwa kipindi hicho, pia kuliambatana ufichuzi wa masakata ya ufisadi wa fedha za umma. Wako watu walijiuzulu wengine walichukuliwa hatua za kisheria. Yote  hayo yalisababishwa na elimu ya uraia kwa wananchi iliyotolewa na vyama vya siasa.

Kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba tuwape moyo vijana wa kujiusisha na siasa za nchi yetu ili kujenga ujasiri katika siasa bila kutazama ni vijana wa chama gani. Tusiwafanye  waione siasa kama mchezo mchafu kama wengine wanavyoamini bali wajue siasa inaamua maisha yetu sote na ni jambo tunalotakiwa kulipa uzito unaostahili. 

Tunatengeneza tatizo halafu tunageuka kuwalaumu vijana tena. Yaani  wakitaka kueleza kuhusu masuala yanayowahusu, tunatumia mabavu kuwanyamazisha halafu baadaye wakiwa wanashindwa kujieleza tunasema vijana wa siku hizi hata kujieleza hawawezi na wamefika vyuo vikuu. Nadhani tunawaonea tuwape nafasi ya kujenga ujasiri wa kuhoji wakiwa katika ngazi za chini kabisa, kuanzia kwenye familia na baadaye shuleni wakijenga utamaduni huo tutapata wasomi wanaojua kujitetea na kulitetea Taifa bila woga wowote, tuwajenge vijana tulijenge Taifa la kesho.

0689157789

[email protected]

Dar es Salaam-Tanzania