Hiki ndicho chanzo cha matatizo ya ndoa nyingi

By Flora Wingia , Nipashe Jumapili
Published at 03:50 PM May 05 2024
Chanzo cha matatizo kwenye ndoa.
PICHA: MAKTABA
Chanzo cha matatizo kwenye ndoa.

KARIBU tena msomaji wangu tuendeleze mada kuhusu mitikisiko katika ndoa nyingi hata kusababisha zingine kubomoka na kila mwanandoa kuanzisha maisha mengine.

Wiki iliyopita tulijadili kwa nini shetani anashambulia sana ndoa? Nilitaja maeneo mawili, moja likiwa ni ujinga kwa baadhi ya wanandoa kutokuwa na maarifa namna ya kuishi katika ndoa.

Nikataja kupuuzia kanuni na misingi ya ndoa. Ukitaka uwe na ndoa yenye mafanikio na upenyo ni lazima utendee kazi kanuni na maelekezo yote yanayohusu ndoa. 

Kwa bahati mbaya sana, watu wengi walioko kwenye ndoa hupuuza na kutupilia mbali kanuni na maelekezo waliyopewa siku wanafunga ndoa. Unapopuuzia kuombea ndoa yako, unapoanza kuona mabadiliko kwa mumeo au mkeo unapuuzia, hiyo itakugharimu baadaye.

Unapoota ndoto mbaya kuhusu mumeo au mkeo na kupuuzia, unaweza kujikuta unaingia kwenye matatizo makubwa ya ndoa baadaye.

Leo msomaji wangu tuende zaidi kuangalia chanzo cha matatizo ya ndoa. Nitajitahidi kuchambua vyanzo mbalimbali kadiri itakavyowezekana ili kusaidia wanandoa wengi ambao wana maswali mengi kuhusu mitikisiko katika ndoa zao wasijue cha kufanya.

Ni vema ikaeleweka kwamba kila tatizo la ndoa lina chanzo. Moja ni zile ndoa zinazofanyika pasipo Mungu kuhusika. (wakati ulikuwa adui wa Mungu). Watu wengi ambao huanza maisha ya ndoa pasipo kumshirikisha Mungu hukumbana na matatizo makubwa ya ndoa.

Siku zote msingi mbaya wa nyumba husababisha jengo kuwa dhaifu. Uhusiano wowote uliofanya wakati ukiwa adui wa Mungu huwa unafeli.

Mwanaume yoyote aliyeokoka na kuchukua maamuzi ua kumuoa binti ambaye hajaokoka, hujisababishia matatizo yeye mwenyewe huko baadaye. Ipo hivyo pia kwa binti kuolewa na mtu asiyeamini upo uwezekano wa matatizo baadaye.

Ndiyo maana Mungu akasema katika moja ya maandiko yake kwamba, “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi?”

Chanzo kingine ni pale ndoa inapofungwa kwa sababu tu ya kupata mimba kwa bahati mbaya/kumpa binti mimba. Watu wengi leo wameoana siyo kwa sababu walipanga, bali kwa sababu walilazimishwa kutokana na kupeana mimba kwa bahati mbaya.

Ndoa za aina hiyo hazifanyiki kwa sababu ya upendo bali kwa sababu ya matokeo ya kile walichokifanya. Aina hii ya ndoa inaitwa “zimamoto”. Kama umewahi kuona watu wa zimamoto wanavyofanya kazi kwa haraka sana na hawana muda wa majadiliano. 

Binti anapopata mimba tu, kila mtu huanza kutaharuki. Wazazi wa pande zote mbili  hukaa kwa haraka na kukubaliana ndoa ifungwe kwa haraka sana ili wasipate aibu.

Aina hii ya ndoa hutokana na tamaa ya mwili na siyo upendo wa dhati. Kama ungekuwa ni wa kweli binti asingejikuta ameingia katika matatizo ya namna hiyo. 

Chanzo kingine ni kujihusisha kimapenzi kabla ya ndoa. Imebaika kwamba mapenzi kabla ya ndoa husababisha matatizo makubwa sana ya ndoa leo na kufanya mtu ajijengee majeneza ya kuzimu. Kama ukijenga jeneza kwa ajili ya ndoa yako, lazima utazikwa huko!

Vijana wengi leo wameshindwa kutunza ujana wao. Mabinti wengi nao wanaaibisha wazazi wao. Wengi wanaingia vyuoni, lakini wanapohitimu wanakuwa ni makahaba waliofuzu!

Chanzo kingine kinatokana na ndoa zilizofungwa baada ya mtu kwenda kwa mganga wa kienyeji. Ni kawaida katika tamaduni za baadhi ya wazazi wa Ki-Afrika kutembelea waganga wa kienyeji ili wawabashirie hatma za watoto wao.

Na mara zote, watu wengine wanaoamini huenda kwa wazazi wao na kuwaambia kwamba Bwana amewaongoza kuoa watu wa aina fulani. Ndipo wazazi huchukua majina ya wachumba wao na kuyakimbiza kwa waganga ili wajue kama ni mke/mume sahihi wa watoto wao.

Kama wewe ni mchunguzi msomaji wangu, wazazi wengi wa ki-Afrika, wana tabia ya kuchukua majina ya watu wanaowazunguka watoto wao. Kama ndoa yako ilifanyika katika misingi hiyo, haitafika mbali. Shetani ni mjanja sana. Anatumia historia ya maisha yako kupambana na maisha ya ndoa.

Leo tuishie hapa tuendelee wiki ijayo, nikutajie vyanzo vingine zaidi vinavyotesa ndoa nyingi katika jamii yetu. Bila shaka umejifunza kitu hapo. Je, una maoni au kisa cha kimaisha? Ujumbe mfupi 0715268581.