Kulikoni kasi wake kukimbia waume zao?

By Flora Wingia , Nipashe Jumapili
Published at 02:43 PM Mar 31 2024
Mawazo.
PICHA: MAKTABA
Mawazo.

KARIBU tena msomaji wangu tuendeleze duru letu la Maisha Ndivyo Yalivyo. Bado jicho letu liko kwenye ndoa. Wiki iliyopita nilisema maisha ya ndoa ni safari ndefu. Kuna wakati mtafurahi na nyakati zitawalazimu kulia.

Kuna wakati mtapishana katika uamuzi na wakati maisha ya uchumi wenu yanaweza kushuka. Hapa ndipo  kuvumiliana na kutiana moyo kunahitajika sana.

Aidha, kuna wakati mnaweza kugongana mawazo na wakati mmoja wenu anaweza kuugua. Hapo ndipo upendo wa kujitoa unatakiwa kudhihirika kwa kila mmoja. Ndoa hii itaweza kusimama tu pale wana ndoa watakapokuwa na upendo wa Mungu kwa kushikamana.

Pamoja na ukweli huo, bado wanandoa wengi wamekuwa hawana uvumilivu inapotokea sintofahamu katika maisha yao ya ndoa. Matokeo yake mawazo mbadala huchipuka na kugawanyika, hatimaye kusambaratika.

Msomaji wangu, nikumegee visa viwili vinavyoonyesha ndoa zilizoparaganyika, kisa mwanamume kapigwa kiuchumi. Maisha yalianza vizuri ndiyo maana hata ndoa kufungwa lakini baada ya muda, hali ikawa si hali na matokeo yake ndoa kubomoka.

Wako vijana wawili nilizungumza nao, mmoja wao kupitia ujumbe wa simu ya kiganjani, wakielezea ugumu wa maisha na yale wanayopitia hadi kujikuta wakikimbiwa na wake zao na kubaki njia panda wasijue cha kufanya.

Kijana mmoja aitwaye James (27), mkazi wa Ifaraka mkoani Morogoro, nikiwa natoka kanisani, nilimkuta na mwenzake wakiwa wameketi karibu na gereji ya bajaji. Nikawapatia kipeperushi kuwaalika kwenye kongamano la maombi.

Baada ya kuwashuhudia, nikataka kujua kwa nini wako pale. Ndipo James akafungaka na kueleza yale anapitia. Akasema: “Hapa na rafiki yangu huyu tumezunguka huko na huko kubahatisha kazi lakini hatujafanikiwa. Mimi ni mchoraji wa mabango na kadhalika.

“Wakati mwingine sipati kazi nakosa hela ya kula. Nimeoa na nina mtoto mmoja. Mke wangu baada ya kuona maisha magumu, alivizia sipo akachukua vitu vyote pamoja na kompyuta mbili za kufanyia kazi akatoroka na mtoto kwenda kwao Dodoma.

“Hapa nilipo sina vifaa vya kazi aliondoka navyo. Natamani nipate nauli niende kwetu Ifakara nikauze sehemu ya shamba langu ninunue kompyuta nyingine niendelee na uchoraji na utengenezaji wa mabango.”

Mpenzi msomaji, huyo ndiye James akitafakari maisha. Mkewe kama angekuwa na upendo wa dhati, angejadiliana na mwenzake kuhusu kwenda kwao. Pia asingechukua vifaa vya kazi ili mumewe aendelee kujiimarisha kiuchumi. 

Shida mwanamke hakuwa mvumilivu. Hata hivyo, nilimsaidia kijana huyu nauli akaondoka kwenda Ifakara ambako bado anatafuta mnunuzi wa shamba lake apate mtaji wa kujiendeleza kimaisha.

Kijana mwingine anaitwa Mussa wa huko Chunya mkoani Mbeya. Huyu alinitumia ujumbe mfupi kwenye simu ya kiganjani. Akasema: “Naitwa Mussa nina umri wa miaka 32 nipo hapa Chunya! Naomba msaada wa kiroho popote ulipo. Usiku naota nafanya kazi, nikiamka nimechoka sana. Kila kazi ninayofanya inakufa.

“Mke wangu kashanikimbia kitambo. Nikiahidiwa kazi inaahirishwa. Nina ujuzi wa kazi saba lakini kula yangu tu ni shida. Kiufupi nina nuksi hatari! Naombeni msaada ndugu zangu mnisaidie”, anamaliza ujumbe wake.

Mpenzi msomaji, bila shaka umepata picha kwa yale wanayopitia vijana hawa wawili. Tatizo kubwa sana ambalo mwanadamu anaweza kupitia katika maisha yake ni tatizo la ndoa. Ni rahisi kukabiliana na changamoto ya biashara lakini si rahisi kukabiliana na mafarakano katika ndoa.

Mungu ameshaweka bayana kwenye moja ya maandiko yake kwamba “mwanamke ni mlinzi wa mume”. Ni “msaidizi”, Mungu alipomuumba mwanadamu wa kwanza, Adamu, alimpatia mwanamke, Hawa, kuwa msaidizi wake kumuondolea upweke.

Hii ina maana kwamba pale mwanaume anapooa halafu mwanamke akaondoka, maisha hupwaya kwani hana msaidizi wala ulinzi. Shetani ndiye kinara wa kumshawishi mwanamke ili atengane na mume wake.

Ndiyo maana tunaweza kuona kwamba matatizo makubwa katika ndoa za watu wengi yana chimbuko refu sana la ki-shetani. Wengi wanaopitia matatizo makubwa ya ndoa hawajui kuwa nguvu za giza zimeachiliwa kuua hatma za maisha yao.

Mwanamke badala ya kuikimbia ndoa, yampasa kupiga magoti kumsihi Mungu aingilie kati kuokoa ndoa hiyo. Bila shaka msomaji umejifunza jambo hapo. 

Je, una maoni, kisa, ushauri? Ujumbe 0715268581. Na hii pia ipo WhatsApp.