Mimi na mume wangu ndoa iliyeyuka jumla!

By Flora Wingia , Nipashe Jumapili
Published at 04:19 PM Mar 24 2024
Wanandoa wakivishana pete.
PICHA: MTANDAO
Wanandoa wakivishana pete.

KARIBU msomaji wangu tuendelee kudadavua vituko ndani ya ndoa zetu. Kila ndoa unayoiona ina changamoto zake. Na kila tikisiko kwenye ndoa lina chimbuko au chanzo chake. Hakuna kinachotokea kwa bahati mbaya.

Maisha ya ndoa ni safari ndefu. Kuna wakati mtafurahi na kuna  nyakati zitawalazimu kulia. Kuna wakati mtapishana katika uamuzi na wakati mwingine maisha ya uchumi wenu yanaweza kushuka uu kugongana mawazo au mmoja wenu aweza kuugua. Hapo ndipo upendo wa kujitoa unatakiwa kudhihirika kwa kila mmoja wenu.

Katika nyakati tunazoishi, yamekuwapo matatizo makubwa sana ya ndoa. Ndoa nyingi sana ziko katika hatua ya kufa au zilishakufa kabisa au wana ndoa wameshafungasha virago na ndoa zao kuzitupilia mbali kabisa.

Wanaume na wanawake wengi sana leo wanajitahidi kutafuta mbinu mbadala za kujiridhisha wao wenyewe kwa kuwa wameshindwa kabisa katika ndoa zao! Hebu sikia kilio cha mama huyu kwa yale aliyopitia kwenye ndoa yake aliyoipenda lakini akaitosa baada ya mambo kumfika shingoni.

Anasema hivi kupitia ujumbe kwenye WhatsApp yangu: “Mume pamoja na kuwa tulifunga ndoa nzuri, nilimfumania ndipo tukaachana moja kwa moja. Hatukwenda  mahakamani wala kanisani kuvunja ndoa na mchezo ukaishia hapo.

Lakini kabla ya kuachana nilitengana naye, nami kwenda kupanga chumba. Hili ni tatizo linalowapata kinamama wengi sana lakini matukio mengine yanaamuliwa kimya kimya.” Huyu mama ni mkazi wa Ngaramtoni ambaye  nilimkuta kwa rafiki yangu hivi majuzi.

Kaka mmoja naye baada ya kusoma makala ya wiki iliyopita, akanitafuta kunimegea kisa cha dada yake ambaye alinasa meseji za simu ndani ya simu ya mumewe na alipomwuliz,a mume huyo akawa anakana.

Katika hali iliyoonyesha ni kweli alikuwa akidhulumu ndoa yao baada ya kumshtukia, sasa akawa analalia simu chini ya mto ili mkewe asizipate na kuzichunguza.

Kwa maelezo yake anasema: “Dadangu ni mjasiriamali, ana duka lake la nguo Kariakoo. Mumewe ni injinia kampuni ya ujenzi. Ni wanandoa na tayari wana mtoto mmoja. Kabla ya ndoa, wawili hawa walipendana sana. Lakini matatizo yalianza mara tu baada ya mtoto kuzaliwa ambapo mume alianza vitimbwi. 

“Mara aanze kurudi saa nane usiku, mara saa tisa na wakati mwingine alfajiri. Akiulizwa na mkewe hajibu. Siku moja akarejea akiwa amelewa sana, hivyo akajisahau mkewe akawahi simu mojawapo. Alipoipekua akagundua meseji kibao za mahaba. Akaamua kunakili namba za simu kisha kesho yake akaipiga namba ile kumwuliza kuhusu meseji zile.

“Mwanamke mwenye namba ile alipopigiwa akajibu kwa jeuri, matambo na matusi juu. Akasema kwani ndoa ni kitu gani. Ilibidi dada yangu amwulize mumewe kuhusu mwanamke huyo wa nje lakini akawa mkali na kukataa kwamba si kweli.

“Akadai ni mfanyakazi mwenzake na pia bosi wake, hivyo asimvunjie heshima. Na mkewe akamwambia kama ni bosi wako lazima niende kumwuliza lakini baada ya hapo mchezo ule ukajirudia.

“Yule bwana kuona mambo ni hadharani akawa mpole kwa takriban siku nne hivi baada ya kuona dadangu kachachamaa. Hata hivyo, alipoona mkewe ameshamshtukia akabadili simu akanunua zile za slid (kutelezesha vidole) ambazo dadangu hajui kuzitumia.”

Swali ni je, kubadilisha simu ili mwenzio asijue yanayoendelea chini ya pazia ni ufumbuzi wa tatizo au unalizidisha? Ukweli ni kwamba tunahitaji sana msaada wa ki-ungu. Hali hii imekuwa ikisononesha sana.

Eneo hili la ndoa si la kupuuzia kabisa. Lazima tukae chini na kuanza kuchimbua jambo hili linalowatesa watu wengi. Pale tu tutakapogundua chanzo cha matatizo ya ndoa, nina hakika tutapata msaada kutoka kwa Mungu mwenyewe utakaobadilisha maisha yetu ya ndoa.

Katika eneo hili tunahitaji hekima ya Mungu, maana hekima ya binadamu haiwezi kutatua matatizo haya. Suluhu ya matatizo ya ndoa huanza pale tu mtu anapomruhusu Mungu kuingilia kati tatizo hili la ndoa. Hakuna tatizo la ndoa linaloweza kumshinda Mungu!

Huenda umeteseka kwenye ndoa yako kwa muda mrefu, huenda umeshakata tamaa kuhusu ndoa yako na labda umeapa hutakaa ujihusishe na mambo yoyote yanayohusu ndoa. Usiogope, Mungu anakwenda kjubadilisha ndoa yako!

Je, una maoni, ushauri au kisa cha kimaisha? Ujumbe 0715268581. Namba ipo kwenye WhatsAPP.