Tumia mitandao ya kijamii huku ukiitazama kesho yako

By Magabilo Masambu , Nipashe Jumapili
Published at 05:40 PM Apr 07 2024
Mitandao ya kijamii.
PICHA: MAKTABA
Mitandao ya kijamii.

NI kweli kwamba mitandao ya kijamii kama facebook, Twitter, Youtube, Whatsapp na Instagram, imerahisisha sana mawasiliano yetu. Leo kwa kutumia mitandao hiyo, tunaweza kuwasiliana na mtu yeyote duniani. Tunaweza kutuma ujumbe (sms), kutuma picha ama video au kupiga simu na kufanya mazungumzo.

Nje ya mawasiliano, wako wanaoitumia mitandao hiyo kibiashara ama kuuza bidhaa zao moja kwa moja, kutangaza au kufanya mawasiliano na wafanyabiashara wengine duniani. Lakini pia inatumika kuonyesha uwezo na vipawa vyetu. Mfano, kama una kipawa cha uimbaji, uigizaji, uandishi, siasa na kila aina ya sanaa, unaweza kuwaonyesha watu uwezo wako kirahisi.

Kinachosikitisha ni kwamba, pamoja na faida zote hizo, wako wanaoamua kwa hiari yao kutumia mitandao ya kijamii kinyume cha maadili yetu ya Watanzania ama kwa kujua au kwa kutojua madhara yake ya leo na kesho. Wanatuma picha au video za utupu mitandaoni bila kujali kwamba wana ndugu, jamaa na marafiki watakaozitazama.

Jambo ambalo hatulijui ni kwamba maisha ya mwanadamu ni fumbo kubwa kwa sababu tunajua tulikotoka lakini hakuna yeyote anayejua tunakokwenda. Kwa manenio mengine, hakuna anayeijua kesho yake. Tunaweza kudhani kwamba tulipo tumefika kumbe Mungu ana mipango mingine na sisi. Wako watu ambao wanajiona waimbaji, waigizaji, wachekeshaji, waandishi na kadhalika na wamejiridhisha kwamba maisha yao yatakuwa hayo.

Mipango ya Mungu ni mikubwa huwa anamwinua yeyote. Unaweza kuwa mchekeshaji leo kama Steve Nyerere kesho ukawa Rais wa nchi kama alivyo Rais wa Ukraine, Volodyymyr Zelensky. Unawezab kuwa mchezaji mzuri wa mpira leo kama Mbwana Samatta,  kesho ukawa Rais kama George Weah wa Liberia. 

Unaweza  kuwa mwanamitindo leo kama Hamisa Mobeto kesho ukawa  Jokate Mwegelo.  Unaweza  kuwa mwanamziki leo kama Giggy Money kesho ukawa mbunge kama Mwana FA.  Wako wengi ambao walikuwa watu wa kawaida lakini wamekuwa maarufu na wameshika nafasi nyeti. Kwa mantiki hiyo, yeyote anaweza kuwa chochote.

Ninachotaka kusema ni kwamba nafasi tulizo nazo leo tusione hatuwezi kuwa wengine kesho. Kwa maana hiyo, matukio tunayoyafanya tukiwa na nafasi tulizo nazo leo,  tuyafanye tukiwa waangalifu kwamba kesho na keshokutwa tukiwa watu mashuhuri kwenye jamii, mambo yetu ya leo yasitufanye tukahukumiwa kesho. Ni  mjinga tu atakayehukumiwa kesho utetezi ukawa kwamba, nilifanya hayo kwa sababu nilikuwa msanii au ilinilazimu kufanya hayo kwa wakati huo. Lazima  tutambue kwamba mitandao ya kijamii inahifadhi taarifa zetu milele.

Leo unapiga picha au video za utupu unazituma mtandaoni, kesho unakuwa Rais kama kijana wa Senegal au mtu mashuhuri. Waungwana  wanakukumbusha kwamba kuna kapicha kako hapa unakakumbuka? Unaanza kutumia vyombo vya usalama kuwaumiza wanaokukumbusha kwa mambo ulioyafanya mwenyewe ukiwa na akili timamu. Nani atalaumiwa katika hilo kama si mwenyewe utajilaumu?

Nakubali kwamba kwa sababu ya ukuwaji wa teknolojia, inawezekana ukarekodiwa bila kuwa na taarifa lakini uzoefu unaonyesha wengi wamekuwa wakijirekodi na kupiga picha wenyewe au kuwaamini watu wao wa karibu na kwamba watazitunza. Lakini inapotokea kutokuelewana, wanaona silaha ya kukumaliza ni kuachia picha na video zako. Ni muhimu sana kujilinda kabla ya kulindwa na wengine. Linda  utu wako lakini zaidi heshima yako ya leo na kesho.

Wako wanaotumia picha zao kuongeza watazamaniji (viewers) kwenye mitandao yao ya kijamii na inawezekana inawapatia fedha. Kwa  maoni yangu, bado una uwezo wa kuongeza watazamaji kwa kulinda maadii, utamaduni na utu wako kwa sababu si watazamaji wote wanafurahia kuona picha za utupu. Fedha zinazopatikana kwa njia hiyo, hazitakuwa tofauti na za ukahaba au uuzaji wa bangi. 

Jambo ambalo wengi pia hawajalifahamu ni kwamba leo hii watu wengi wanakosa kazi duniani kwa sababu tu wamekuwa watumiaji wabaya wa mitandao ya kijamii. Unakwenda kuomba kazi kwenye kampuni fulani, una vigezo vyote vya kielimu lakini   wanaotaka kukupatia kazi wanaona wajiridhishe kwa kulitafuta jina lako kwenye mitandao, wanakuta mambo ya ovyo! Maana  yake wanaona wakikupatia kazi, unaweza kuharibu taswira ya kampuni yao. Wanaamua kutokuchukua pamoja na kwamba unazo sifa za msingi. 

Ushauri wangu kwa watumiaji wenzangu wa mitandao ya kijamii, ni muhimu matumizi yetu ya leo yalinde heshima yetu ya kesho. Tunaweza  kuwa na watoto wadogo leo kesho watakuwa watu wazima. 

Tutawapa taabu sana watakapokuwa na wenzao au wenyewe kuzitazama picha na video zetu. Ishi leo kwa matarajio ya kuwapo kesho. Kazi  yako leo isiuwe matumaini ya kuwa mtu mwingine kesho kwa kuwa lolote linawezekana bali ni jambo la muda tu. 

0689157789

[email protected]

DAR ES ALAAM-TANZANIA