Wajane wasimulia magumu malezi watoto bila wenza

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 12:22 PM Mar 24 2024
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maaalum, Dk. Dorothy Gwajima, akizungumza na baadhi ya wajane mwaka 2022.
PICHA: MAKTABA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maaalum, Dk. Dorothy Gwajima, akizungumza na baadhi ya wajane mwaka 2022.

JARIBU kufikiri kuhusu kauli hii ya Katibu wa Chama cha Wanawake Wajane Tanzania (CCWWT), Sabrina Tenganamba (55), akitoa ujumbe mahsusi kwa wanawake walio kwenye ndoa kwa sasa.

Anatumia msemo katika jamii, kitunze ingali hai, kikifa hautakiona tena, akiufafanua kuwa: “Utatamani kaburi lifunguke aamke mara ya pili walau aje akusumbue tu akupige vibao ili mradi watoto waendelee kumwona.”

Ni rai yake akiwa na ushuhuda kwamba waliopoteza waume zao, wanapitia kipindi kigumu kulea watoto walioachiwa, kupata mahitaji na faraja wanapokabiliwa na sonona.

Katika mazungumzo na mwandishi wa habari hii yaliyofanywa Alhamisi wiki hii jijini Dar es Salaam kuhusu mambo mbalimbali yanayosibu wajane, Sabrina aliwataka wanandoa kutambue kuwa wajane pia walipitia changamoto katika ndoa zao.

“Kuna wengine wanasema yamkini wajane mnaishi vizuri sana kuliko sisi ambao pengine wanaume wanatupasua vichwa,  ninataka nikwambie, ninaapa mwanahabari na sisi waume zetu walikuwa wanatupasua kichwa, lakini ogopa sana atakapozikwa.

“Utatamani kaburi lifunguke aamke mara ya pili walau aje akusumbue tu akupige vibao ili mradi watoto waendelee kumwona. Tunachokiomba wanawake wenzetu si kwamba sababu tumebaki wanawake, muwalinde waume zenu na kuwaombea.

“Ujane ni afadhali upate Corona (UVIKO -19) au Ebola. Afadhali upate ugonjwa wowote mkali ukajua kwamba nitautibu vipi. Ujane hauna tiba, wengine wanasema utapata tiba kwa kuwa na mwanamume mwingine. Hapana. Mtoto anamhitaji baba. Hata yule mgumba anatamani labda mume wake wa ndoa angekuwapo, lakini hayupo. Niwaambie tu mtoto anahitaji baba asikwambie mtu.

“Wenye ndoa mtafute mbinu ya kuweza kutulia kwenye ndoa zenu. Ninamaanisha wanawake watulie kwa ajili ya watoto. Wanyamaze kimya. Wasiombee kwamba afadhali angekufa. Hapana. Kitunze kingali hai, kikifa hautakiona tena,” alisema.

MALEZI BILA WENZA

Sabrina anaainisha changamoto kubwa ambazo zinawakabili wanawake hao kuwa ni pamoja na kutengwa na ndugu, jamaa na marafiki kwa kukaa mbali na mjane endapo uchumi wake si mzuri.

“Kama una watoto wengi ndugu wanaogopa kuelemewa. Hii ni changamoto kubwa sana kwa wale ambao hawajaachwa vizuri. Ameachwa hana mali kwa lugha rahisi ni maskini.

 “Hali za wajane ni uwiano wa 50/50. Wako walioachwa wakiwa tegemezi kwa waume zao lakini pia, wako ambao walinyang’anywa mali baada ya waume zao kufa na baadhi huogopa kwenda mahakamani. Lakini katika miaka hii mitatu iliyopita, mwamko wa wajane kudai haki umeongezeka,” alisema.

Sabrina alisema kwa upande wa vijijini suala la mjane kupigania mahakamani haki ya mali alizoachiwa na mume bado ni tatizo. Alibainisha kuwa baadhi wakikabiliwa na uoga wakihofia kusimama na mashemeji katika mahakama.

KESI KUCHELEWA

Katibu huyo anataja changamoto nyingine ni wajane kukaa katika kesi miaka mingi bila kupata haki zao na mwisho wa siku kupoteza umiliki.

“Changamoto nyingine ni mjane anakuwa na kesi ya mirathi au ya madai. Pengine  mume alikopa akaacha deni unakuta kesi inachukua miaka mingi na hapo anajikuta anatumia gharama za kwenda na kurudi mahakamani.

“Kuandika tu barua kwenda mahakamani inahitaji fedha, kutafuta wakili inahitaji fedha na hali hii wengine huishia kupata kiharusi au kupoteza mali kabisa hata kama ana haki.

“Hii changamoto ya kesi kukaa muda mrefu kama hana wakili imesababisha baadhi kukata tamaa. Kipo Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) wanatusaidia sana lakini unakuta kuna muda mjane mwenyewe anapokwenda kwa wakili anayemsaidia bure bado atalazimika kutumia fedha mfano nauli.

“Wengine wanakata tamaa kutokana na kesi kuchukua miaka mingi. Kuna mwanachama wetu ana kesi ina miaka 40 na yeye ana umri wa miaka 78 sasa. Kesi yake ni ya madai ya kudhulumiwa na rafiki wa mume wake maghorofa aliyoachiwa na mume wake.

“Mwingine ana kesi ambayo ina takriban miaka 20 mahakamani inahusu mkopo ambao mume wake alichukua benki. Kesi nyingine ambayo sasa ina miaka 15 ni ndugu wa mume wamekuwa wakikata rufani dhidi ya mjane kuhusu mali,” alisema.

Pia alisema wajane walio wengi wanakabiliwa na changamoto ya mitaji hasa wenye umri wa miaka 55 kushuka chini na hiyo inatokana kukosa mali isiyo hamishika kutokana na kuachwa katika nyumba za kupangisha.

WOSIA

Sabrina alisema baadhi ya wajane waliowapokea katika chama, waume zao kabla hawajafa waliacha wosia lakini ndugu walipojaribu kupora haki, walikwama kwa sababu serikali inasimamia uamuzi wao, wengi wanapata wanachostahili.

“Baadhi hudhani wosia ni kama mjane ameuandika mwenyewe ili kupata mali na wengine huuchukulia kama mjane amekusudia kuua mume ndiyo maana alilazimisha kuandikwa wosia. Tunasisitiza sana hasa wale ambao hawajapata majanga na wanaume ambao waliopo katika ndoa wafahamu kuwa, wosia si kifo,” alikumbusha.

SIMULIZI YAKE

Sabrina anafunguka kuhusu safari ya maisha yake kuwa: “Mimi mwenyewe nimeandika wosia kwa ajili ya watoto. Husaidia wale wanaobaki nyuma. Hatujui anatangulia baba au mama.

“Anaweza kutangulia yeyote. Wosia husaidia kutatua tatizo kwa jamii inayobaki hai hata ugomvi hautakuwapo wala mambo ya mahakama mara kwa mara hayatakuwapo. Hata sisi ndani ya chama tunasisitizana kuandika wosia,” anaelimisha.

“Binafsi mume wangu ameniachiwa watoto watano na nina wajukuu wanane kwa sasa. Ninaishi eneo la Abiola huko Yombo, Temeke mkoani Dar es Salaam. Mume wangu hakuniachia mali. Nilizo nazo nimetafuta mwenyewe. Kifo chake kilitokana na ajali. Mimi na mume wangu tulinunua gari jipya tulipata ajali yeye alifariki dunia papo hapo.

“Ndugu wa mume walinitenga nikaonekana kisababishi cha kifo chake. Ndugu hawako karibu sana wa watoto wangu. Katika ajali ile iliyotokea mwaka 2004 niliumia mkono wa kulia ambao haufanyi kazi. Mume wangu akaniacha na watoto,” anasimulia.

TAWLA

Mkurugenzi Mtebndaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Wakili Tike Mwambipile, akifafanua kuhusu masuala ya kisheria na ucheleweshaji wa kesi uliolalamikiwa, alisema miaka ya hivi karibuni, mahakama ilitengeneza utaratibu kuhakikisha majalada hayachukui muda mrefu mahakamani.

“Kuchukua muda mrefu inategemea kama ilianzia mahakama za chini. Ila kuna jitihada ambazo zimewekwa na mahakama kuhakikisha kesi zinazoletwa zinasogea kwa haraka ili watu wapate haki zao.

“Zamani ndio kulikuwa na ucheleweshaji. Hii hatupingi lakini mfumo wa sasa wa kimahakama, unatambua na unategemea na kesi ina mambo gani ndani yake, lakini nyingi ndani ya miaka miwili zinatakiwa ziwe zimekamilika,” alisema. 

Wakili Mwambipile alisema katika masuala ya mirathi, ni changamoto ambayo huanzia kwenye sheria zilizoko zinazoangalia suala hilo. Alisema nchi ina sheria tatu za masuala ya mirathi ambazo ni sheria ya Kiislamu, sheria za kimila na sheria za kiserikali.

“Hiyo pia unaangalia maisha aliyoishi marehemu. Inachanganya ndiyo maana wanaharakati wengi na chama unachokisema (CCWWT) kwa umoja wetu tunataka sheria ifanyiwe marekebisho na kuwa na sheria moja ambayo inatizamwa kwa mapana.

“Ukitumia za sasa, mtu akienda kimila kuna watu watanyimwa haki zao wakati wanastahili kupata. Mapendekezo yetu ya sheria moja tunataka wale warithi halali wa marehemu wapate mali zao kihalali. Tumewahi kupeleka Sheria Pendekezwa serikalini kwamba, mfano wa sheria na Wizara ya Katiba na Sheria inayo huo mfano,” alisema.

Kuhusu suala la wosia, alisisitiza ni muhimu kwa kuwa kulingana na changamoto ya sheria hizo mtu anapokuwa na wosia ndio utakaosaidia kupata haki kwa warithi halali kama ilivyoandikwa na hautaacha ugomvi.

ITAENDELEA KESHO…