Bashe ataja mageuzi sekta ya umwagiliaji

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:49 PM May 02 2024
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Picha: Augusta Njoji
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

SERIKALI kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa mwaka 2024/25, imepanga kukarabati ya miundombinu ya umwagiliaji kwenye skimu 33 zenye hekta 6,089 zitakazonufaisha wakulima 4,693.

Pia, Tume itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde ya kimkakati yenye takribani hekta 255,181.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akiwasilisha bungeni leo makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka huo, amesema pia NIRC, itafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa kutumia maji ya ziwa Victoria kwa ajili ya shughuli za kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji na mikoa itakayonufaika ni  Simiyu, Shinyanga, Tabora,  Singida na ziwa Tanganyika kwenye mikoa ya Kigoma na Katavi.

Amesema Tume hiyo kwa kipindi hicho itaendelea na utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji 780 iliyoanza kutekelezwa mwaka 2022/23 na 2023/24 ambayo ni kukamilisha utekelezaji wa miradi 69 ya ujenzi na ukarabati ambayo ilianza mwaka 2022/23 inayojumuisha ujenzi wa mabwawa 14 yenye mita za ujazo milioni 131.5.