Elimu ya fedha kufundishwa elimu msingi, vyuo vikuu

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 06:23 AM Apr 19 2024
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga.

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wanatarajia kutoa elimu ya fedha kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu.

Lengo likiwa ni kuwawezesha vijana kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na kufahamu namna ya kuzitunza.

Akizungumza jana jijini Dar es salaam wakati akifungua warsha kuhusu uchopekaji wa elimu ya fedha katika mitaala ya elimu ya juu, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga alisema serikali imedhamiria kujenga uelewa wa masuala ya fedha kwa jamii.

Alisema BoT itaendelea kusimama na vyuo na taasisi za elimu na Wizara ya Elimu katika kuhakikisha dhana ya elimu hiyo inakuwa endelevu na inafundishwa katika ngazi za jamii.

Aidha, aliviagiza vyuo vikuu kushirikiana na BoT kufanya tathmini ya utekelezaji wa mpango huo ili kuboresha mbinu na nyenzo za kufikisha ujumbe huo kwa jamii.

Naibu Gavana wa BoT, Sauda Msemo alisema elimu ya fedha inakuwa ni sehemu ya masomo itakayofundishwa ngazi zote kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo vikuu.

Alisema: “Aprili mwaka jana BoT iliwashirikisha wakuu wa taasisi za elimu ya juu nchini, kwa  uwakilishi wa wakuu wa  vyuo vikuu pamoja na TCU na NACTIVET kwa lengo la kukubaliana juu ya azma ya kufundisha somo la elimu ya fedha  ngazi ya elimu ya juu nchini”.

Aliongeza: “Hadi sasa taasisi tatu za elimu ya juu zimechukua hatua za kuingiza somo la elimu ya fedha katika mitaala yao, hivyo warsha hii itachochea uwepo wa elimu  ya fedha kwa vyuo vingi nchini kuendana na mabadiliko ya mageuzi ya kiuchumi nchini”

Sauda alisema takwimu ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 inaonesha asilimia 34.5 ya Watanzania ni vijana walio na umri kati ya miaka 15-35.

Alisema ili kuleta tija na ufanisi katika masuala ya uchumi  ujuzi na uzoefu wa masuala ya fedha ni moja ya sifa muhimu kufikia azma hiyo.

Alisema elimu ya fedha kwa Watanzania itachochea maendeleo kwa kuongeza utumiaji rasmi wa huduma za fedha na kuwawezesha watu wengi kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi na kukuza uchumi kwa ujumla.

Sauda alisema elimu kwa vijana wa vyuo vikuu itawasaidia kuweka akiba, kupanga bajeti na kufanya uamuzi wa masuala ya fedha kwa kuzingatia viashiria hatarishi na kuelewa taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za fedha ili kufanya maamuzi sahihi ya fedha ili waitawale.

Pia, alisema BoT kwa kushirikiana na wadau wengine wa Baraza la Huduma Jumuishi za Fedha, imetoa mwongozo na mtaala wa elimu ya fedha kwa wakufunzi ambao utatumika na taasisi za elimu ya juu kwa kuwafundisha watoa huduma za elimu ya fedha kuwafikia wananchi.