Mawakala mbolea wafundwa elimu ya sheria, utoaji huduma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:16 AM Apr 30 2024
Mbolea.
Picha: Maktaba
Mbolea.

MAWAKALA wa kuuza na kusambaza mbolea wamepewa elimu ya sheria na utoaji wa huduma bora kwa wakulima ili kuongeza tija katika sekta ya kilimo.

Akizungumza wakati wa utoaji elimu hiyo, Meneja wa Mamlaka ya Uthibiti Mbolea Tanzania (TFRA) Kanda ya Ziwa, Michael Sanga alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwapatia uwezo mawakala hao.

Alisema kinachotakiwa ni kuhakikisha wanatoa huduma bora ili kuepukana na vitendo vya udanganyifu kwa wakulima hasa katika uuzaji wa mbolea zisizo na viwatilifu imara.

Alisema ni vyema wakulima wakapata ushauri kutoka kwa wasambazaji wa mbolea ili kutambua aina ya viwatilifu vya kutumia kulingana na mazingira husika wakati wa kilimo.

"Nawaombeni muweke mifumo rafiki ya kuwaelimisha wakulima kununua mbolea kwani matumizi ya mbolea kwa Kanda ya Ziwa yapo chini ukilinganisha na mikoa mingine hapa nchini, nyie wauzaji mnapaswa kutoa elimu kupitia mashamba darasa pamoja na viongozi wa serikali kuhimiza matumizi ya teknolojia katika matumizi ya mbolea," alisema.

Aidha alitoa wito kwa kampuni za mbolea kuendelea kufungua vituo vikubwa vya kusambazia mbolea katika vituo vya kanda ili kusaidia wafanyabiashara kuvuna mazao mengi.

Mkuu wa Idara ya Masoko wa Kampuni ya Mbolea MINJINGU, Dk. Mshindo Msolla alisema ni vyema wakulima kuwa na utaratibu wa kusema matatizo yao mara kwa mara ili serikali na kampuni za kusambaza mbolea waweze kujua namna bora ya kuboresha huduma.

Lydia Mtani ni mmoja kati ya washiriki wa mafunzo hayo alisema baadhi ya wakulima wanamwamko mdogo kuhusu kilimo kunakosababishwa na elimu ya kutumia mbolea na ukosefu wa shamba darasa.

Elias Tilya alisema wakati wa mvua kunasababisha mbolea kuhama pamoja na suala la usafiri imekuwa ni tatizo katika usafirishaji wa mbolea jambo linalosababisha mawakala kutokutoa huduma bora kwa wakukima.