Wataalamu wa miwa waishauri serikali kuboresha utafiti

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 09:30 AM May 07 2024
Miwa.
Picha: Maktaba
Miwa.

WATAALAMU wa miwa na sukari Tanzania wameishauri serikali kuendelea kuboresha huduma za utafiti na mazingira ya uwekezaji ili kufikia lengo la uzalishaji wa sukari nchini kutokana na sekta hiyo kukabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa uhakika wa mbegu za miwa zinazofaa kwa uzalishaji wa sukari.

Hali hiyo inatajwa kuwa ni changamoto kubwa licha ya jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na serikali katika kukabiliana na changamoto za sekta hiyo ikiwamo bei na upatikanaji wa uhakika kutokana na karibu asilimia 90 ya mbegu zinazofaa kuzalisha miwa inayofaa kwa sukari kuagizwa nje ya nchi.

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Chama cha Wataalamu wa Miwa na Sukari Tanzania (TSCCT), Fedrick Charles, alisema hayo kwenye kongamano la 10 linalokutanisha wataalamu mbalimbali wa sekta hiyo kutoka viwanda vyote vya sukari nchini ikiwamo Kilombero Sugar, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, TPC, Mkulazi Holding Company, Bagamoyo Sugar na taasisi nyingine zote zinazojihusisha na sekta hiyo.

Alisema ukosefu wa mbegu za kisasa zenye kiwango kikubwa cha sukari unasababisha wamiliki wa viwanda kuagiza mbegu hiyo nje ya nchi hasa katika nchi za Afrika ya Kusini, Mauritius, Malawi na nchi zingine.

Alisema ili kuongeza tija mashambani na utoshelevu wa sukari nchini ipo haja ya kuwa na maabara ya kutafiti kwa ajili ya kuangalia afua ya udongo, viatilifu na mbegu zinazoendana na ikolojia.

Changamo nyingine walizozibainisha wataalamu hao wa sukari ni ukosefu wa mashine mbalimbali za viwandani na zinazo sababisha pia kuagizwa nje ya nchi na kuongeza gharama za uzalishaji hali inayopandisha bei ya sukari pamoja na maabara ya kufanya uzalishaji wa mbegu ‘planting breeding’.

"Ndio maana tunawasihi wadau mbalimbali wa sekta ya sukari kuona fursa ya uwekezaji wa vifaa hivyo hapa nchini kutokana na uhitaji wake kuendelea kukua siku baada ya siku, lakini ili kuwe na kilimo endelevu cha miwa ya sukari inahitajika teknolojia ya kisasa ya umwagiliaji na uvunaji wa kutumia mashine za kisasa," alisema.

Hata hivyo, alisema bado nchi imeendelea kufanya jitihada mbalimbali kukabiliana na changamoto katika sekta ya miwa na sukari ikiwamo kuwekeza kupata wataalamu wengi.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, George Gowele, alisema mikakati mbalimbali inayoendelea kufanywa na serikali ili kuondoa changamoto hiyo ya mbegu ikiwamo jitihada kubwa kupitia Wizara ya Kilimo na Taasisi ya Utafiti wa Mbegu nchini TARI kituo cha Kibaha ili kuendana na uhitaji.

Alisema jitihada hizo zimeanza muda mrefu tangu mwaka 2005 na tayari kuna mbegu ambazo tayari zimeandaliwa ikiwamo aina ya Tariska 121-122 ambazo tayari zimeanza kuoteshwa kwa majaribio katika maeneo mbalimbali.

Jitihada zingine ni uanzishwaji wa vitalu vya mbegu katika kiwamda cha Sukari Mtibwa kwaajili ya wakulima wadogo na Mkoa wa Manyara vitakuwapo vitalu kwa lengo la kuondoa changamoto ya mbegu za miwa nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, alisisitiza wataalamu hao kutambua kuwa wao ni jicho la taifa katika sekta ya sukari na lazima waweke nguvu kuondoa changamoto zilizopo. 

Alitoa wa mfano hali iliyopo sasa ya mabadiliko ya hali ya hewa na namna yanavyoathiri ukuaji wa sekta hiyo na kwamba ni vyema kuwa wabunifu na kutumia teknolojia za kisasa ili kwenda sambamba na malengo ya nchi.